• HABARI MPYA

    Monday, September 10, 2012

    SAFU YA USHAMBULIAJI SIMBA YATIMIA KUIBOMOA AZAM KESHO

    Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    MSHAMBULIAJI mpya wa Simba SC, Daniel Akuffo kutoka Ghana, yupo fiti kwa asilimia 100 kucheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kwa ujumla timu haina majeruhi.
    Akuffo aliumia Alhamisi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Sofapaka ya Kenya, ambao Simba SC walifungwa kwa mabao 3-0, mshambuliaji huyo kutoka Hearts Of Oak ya Ghana akishindwa kumaliza dakika 45 tu za kwanza baada ya kuumia vibaya kiasi cha kupoteza fahamu.
    Daktari wa Simba SC, Cosmas Kapinga ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, baada ya Akuffo kupata mshituko mkubwa kwa kuchezewa rafu mbaya ghafla siku hiyo kiasi cha ulimi kugeuka na kupoteza fahamu, alipatiwa tiba na makini na siku iliyofuata akawa fiti kabisa.
    Daktari huyo wa mabingwa wa Tanzania Bara, alisema kwamba klabu hiyo haina majeruhi zaidi na wachezaji wanaokosekana kwa sasa ni washambuliaji Mzambia Felix Sunzu ambaye kwenye mazishi ya dada yake na Emmanuel Okwi ambaye yupo na timu ya taifa ya kwao, Uganda. 
    Simba ipo kambini hoteli ya Sapphire, Kariakoo ikijiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC kesho na Akuffo aliyeifungia Simba katika kila mechi, kwenye tatu za kirafiki ilizocheza ikiwa kambini Arusha, dhidi ya Mathare United, (2-1), JKT Oljoro (2-1) na Sony Sugar (1-1) anategemewa sana kuifutia uteja timu yake mbele ya Matajiri wa Chamazi.  
    Habari njema zaidi mshambuliaji mwingine hatari wa Simba SC, Emanuel Arnold Okwi ametua jana kutoka Zambia, ambako aliichezea timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini jana na kufungwa 1-0 kwa mbinde. 
    Okwi alitua Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere saa 1:00 usiku huu na moja kwa moja kuingia kambini, hoteli ya Sapphire, Kariakoo ambako klabu yake, Simba SC imejituliza ikijiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC keshokutwa, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Okwi hajaichezea Simba mechi yoyote tangu msimu huu uanze, kutokana na pilika zake za kujaribu kuhamia Ulaya, ambazo hazikufanikiwa.
    Okwi alikaribia kujiunga na FC Red Bull Salzburg ya Wals-Siezenheim, Austria baada ya kufuzu majaribio ya wiki tatu, lakini klabu huyo ikaghairi dakika za mwishoni akarejea nchini.
    Kukwama kwa Okwi kuliikosesha Simba Euro 600,000 ambazo klabu hiyo, ilikuwa tayari kutoa kumnunua.
    Awali, Simba ilipata ofa ya kumuuza Okwi kwa Sh. Bilioni 2 kwa klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, lakini mshambuliaji huyo akasema anataka kwenda Ulaya.
    Awali Olando Pirates ya Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye majaribio huko kama angefuzu wangemsajili dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya Parma.
    Sasa Simba inamsubiri mshambuliaji wake mmoja tu, Mzambia Felix Sunzu ambaye kwa wiki nzima yuko kwao kwenye msiba wa dada yake, ambaye naye anatarajiwa kutua nchini wakati wowote tayari kwa mechi hiyo pia.
    Kihistoria mechi ya kesho itakuwa ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kukutanisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
    Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 

    MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
    Mwaka          Mshindi   Matokeo
    2001               Yanga       2-1 Simba
    2010               Yanga       0-0 Simba (3-1penalti)
    2011               Simba       2-0 Yanga
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAFU YA USHAMBULIAJI SIMBA YATIMIA KUIBOMOA AZAM KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top