• HABARI MPYA

    Saturday, September 08, 2012

    KEITA, OCHIENG WAITWA MAGALASA MAPEMAAA

    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe (kushoto) akimkabidhi jezi ya klabu hiyo, beki Paschal Ochieng mwezi uliopita baada ya kukamilisha usajili. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange 'Kaburu.
    Na Doris Maliyaga USHAURI wa bure kwa Simba. Klabu hiyo si vibaya ikawatumia wakala aliyewasaidia kumpata Mganda Emmanuel Okwi, kusaka wachezaji wa kigeni baada ya raia wa Mali, Komanbilli Keita na Mkenya Pascal Ochieng kuboronga katika mechi ya kirafiki dhidi ya Sofapaka ya Kenya na kupigwa mabao 3-0 juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
    Kiwango cha chini kilichoonyeshwa na Keita na Ochieng kilifanya kocha mzawa, Kenny Mwaisabula ahoji wamefuata nini? 
    Kupwaya kwa Keita na Ochieng kulikuwa na mwendelezo wa makosa ya Simba katika usajili wa wachezaji wa kigeni kwani kabla ya hata ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza msimu huu, ililalizimika kuwatema beki Lino Masombo na kiungo Nkanu Mbiyavanga, ambao walitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 
    Nyota hao, ambao walisajiliwa kutoka Motema Pembe hawakung'ara kwenye Kombe la Kagame wakapandishwa ndege mapema. 
    Katika kuashiria wamejifunza na makosa, Simba walishusha nyota wa hao wa kigeni kuivaa Sofapaka, lakini mambo yalikuwa yale yale na hasa katika upande wa beki, ambayo ilipwaya kwenye Kombe la Kagame. 
    Keita na Ochieng walianza katikati huku Shomari Kapombe na Amir Maftah wakicheza pembeni, lakini walikosa uelewano na kuwafanya washambuliaji Sofapaka watambe. 
    Walicheza pamoja kwa dakika 50 na katika kipindi hicho, Simba waliruhusu mabao matatu. Kati ya mabao hayo moja lilikuwa la penalti iliyotolewa baada ya Keita kuunawa mpira. 
    Mabao mengine mawili yalitokana na mabeki hao wa kati kutokuwa makini, lakini hali ilikuwa tofauti baada ya Juma Nyosso na Said Nassoro 'Cholo'kuingia badala ya Keita na Ochieng. 
    Nyosso alituliza sehemu ya ulinzi baada ya kucheza kama beki wa kati akisaidiana na Kapombe, ambaye alihamishiwa katikati wakati Cholo alichukua nafasi ya Kapombe kama beki wa kulia. 
    Kutokana na hali hiyo, Mwaisabula aliliambia Mwanaspoti kuwa: "Keita na Ochieng hawako sawasawa na ndiyo sababu ya Simba kufungwa. 
    Wamecheza hawaelewani, Keita hatumii akili na anacheza faulo nyingi, nimeshangaa nilipoona kiwango chake kwani mchezaji wa kigeni anatakiwa kuwa na vitu vya ziada. 
    "Naye Ochieng ni mzito tofauti na alivyokuwa Yanga. Unajua watu wanatarajia makubwa kutoka kwa mchezaji wa kigeni," alieleza Mwaisabula. 
    Mghana Daniel Akuffo, ambaye alikuwa ameifungia Simba katika mechi tatu zilizopita, alicheza kwa dakika 38 tu na kutolewa baada ya kuumia. Ingawa hakupiga hata shuti moja lililolenga lango. 
    Hali hiyo inafanya Okwi kuwa mchezaji pekee wa kigeni tishio kwani hata Mzambia, Felix Sunzu ameshindwa kurudia cheche zake za mwaka 2010 alipokuwa anatamba na timu za Lupopo ya Congo na timu ya taifa ya Zambia.


    SOURCE: Gazeti la Mwanaspoti leo
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KEITA, OCHIENG WAITWA MAGALASA MAPEMAAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top