• HABARI MPYA

    Wednesday, January 09, 2013

    CHUJI ASEMA DENIZLISPOR LILIKUWA BONGE LA KIPIMO YANGA JANA

    Chuji ndani ya Uturuki

    Na Prince Akbar
    KIUNGO wa Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’ amesema kwamba Denizlispor FC waliyocheza nayo jana mchezo wa kirafiki kilikuwa kipimo kizuri kwao, kwani timu hiyo ni nzuri zaidi ya ile waliyocheza nayo awali, DSC Arminia Bielefeld ya Ujerumani.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kutoka Uturuki jana, Chuji alisema kwamba mechi ya jana imewasaidia sana kujua mapungufu na ubora wao kwa kuwa walicheza na timu nzuri iliyowazidi uwezo.
    “Hii timu ni nzuri sana, kwa kweli imetupa changamoto nzuri na sisi wenyewe kama wachezaji tumeona hicho kitu,”alisema Chuji.
    Yanga SC jana ilifungwa mabao 2-1 na Denizlispor FC ya Denizli, nchini Uturuki katika mchezo wake wa pili wa kujipima nguvu katika ziara yake ya Uturuki, bao la kufutia machozi likifungwa na Jerry Tegete.
    Pamoja na kufungwa na timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, iitwayo Bank Asya 1. Lig, ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 10, imeelezwa Yanga ilicheza soka ya kuvutia.
    Denizlispor Football iliyoanzishwa mwaka 1966, inatumia Uwanja wenye kuingiza mashabiki 19,500 wa Denzili Ataturk na mafanikio yake makubwa hivi karibuni ilikuwa mwaka 2002 waliposhika nafasi ya tano katika Ligi Kuu ya nchini humo na kufuzu kwenye mchujo wa Kombe la UEFA.
    Mwaka huo, ilifanya maajabu kwa kuzifunga timu zenye majina Ulaya kama FC Lorient, Sparta Prague na Olympique Lyonnais, kabla ya kufungwa katika Raundi ya Nne na FC Porto ya Ureno, ambao walitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwishowe.
    Katika mchezo wake wa kwanza wa kujipima nguvu, Yanga ilitoka 1-1 na DSC Arminia Bielefeld ya Ujerumani, bao la timu hiyo ya Jangwani likifungwa na Tegete.
    Kikosi cha Yanga jana kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdu, Kabange Twite, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Nurdin Bakari, Jerry Tegete/Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi/Hamisi Kiiza na Simon Msuva.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: CHUJI ASEMA DENIZLISPOR LILIKUWA BONGE LA KIPIMO YANGA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top