Monaco yataka kuwang'oaNasri na Tevez Manchester City
Feb 9, 2013 10:45:00 PM
VINARA wa Ligi Daraja la Kwanza Ufaransa, wakiwa wanajiandaa kurejea Ligi Kuu, wamepanga kuchukua nyota wawili wa mabingwa wa Ligi Kuu, ili kuimarisha kikosi chao kwa dau la Euro Milioni 41.
KLABU ya Monaco inawataka wachezaji wa Manchester City Samir Nasri na Carlos Tevez kwa dau la Euro Milioni 41 mwishoni mwa msimu.
Dhamira ya vinara hao wa Ligue 2 ni kurejea kwenye matawi ya juu ya soka ya Ufaransa baada ya kushuka mwaka 2011 na bilionea Dimitry Rybolovlev, ameonyesha dhamira ya kuwanasa wawili hao kutoka kikosi cha mabingwa wa England.
Mfanyabiashara huyo wa Kirusi, anayeshika nafasi ya 93 kwa utajiri duniani, amepania kupambana na matajiri wengine wa Ufaransa, Paris Saint-Germain katika matumizi ya fedha ili kujenga kikosi tishio.
Monaco ilijaribu bila mafanikio kumnasa kocha Roberto Mancini msimu uliopita licha ya kumpa ofa ya mshahara wa Euro Milioni 8.2 kwa mwaka, lakini inaamini itafanikiwa kuwapata Tevez na Nasri, ambao kwa sasa hawana nafasi kwenye kikosi cha kwanza Uwanja wa Etihad.