![]() |
Na Bin Zubeiry |
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Jumatano ilikibwaga kigogo cha soka Afrika, Cameroon bao 1-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shukrani kwake, mshambuliaji wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Ally Samatta, aliyeifungia Tanzania bao hilo pekee la ushindi katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa, uliovuta hisia za mashabiki wengi nchini.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager pia, alifunga bao hilo dakika ya 89, baada ya kwanza kuvunja mtego wa kuotea wa mabeki wa Cameroon, kisha kumchambua kipa wa mabingwa hao wa Olimpiki mwaka 2000, Effala Komguep kufuatia krosi maridadi ya Salum Abubakar 'Sure Boy'.
Sama Goal alitumia akili ya hali ya juu kufunga bao hilo, baada ya kuwekewa ulinzi mkali kwa muda wote wa mchezo, kwani alifanya kama hawanii mpira na ghafla akauchomokea, wakati mabeki wa Simba Wasiofungika, wakidhani kipa wao atauwahi.
Aidha, kwa bao hilo tamu, ni sawa na Samatta au Poppa kuwaomba radhi mashabiki kwa kitendo chake cha kususia kambi ya timu iliyokuwa ikijiandaa kucheza na Zambia.
Huu ni ushindi wa tatu mfululizo wa nyumbani kwa Taifa Stars, baada ya awali kuzifunga Kenya Novemba na Zambia Desemba, zote 1-0.
Stars ingeweza kuondoka na ushindi mnene Jumamosi, iwapo beki Erasto Nyoni angefunga penalti dakika ya 25, lakini kipa Komguep aliipangua.
Penalti hiyo ilitolewa na refa Munyemana Hudu wa Rwanda baada ya beki Ngoula kumchezea rafu Samatta kwenye eneo la hatari.
Mchezo huo, ulikuwa maandalizi kwa Stars kabla ya kucheza na Morocco mwezi ujao Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
Kiufundi, katika mchezo wa Jumatano Stars imeonyesha matumaini makubwa kutoana na kuendelea kubadilika kiuchezaji kwa kasi.
Siku hiyo ilishuhudiwa nidhamu ya hali ya juu kiuchezaji kuanzia safu ya ulinzi, kiungo hadi washambuliaji.
Stars siku hiyo hawakucheza ovyo, walicheza kwa mipango na kuepuka kuingia kwenye mitego ya Cameroon.
SAFU YA ULINZI:
Kipa na Nahodha Juma Kaseja Jumatano alitulia mno langoni na kucheza kwa maelewano makubwa na safu yake ya ulinzi.
Alicheza krosi vizuri, aliokoa michomo kadhaa na aliweza kuitokea vema mipira na kuinyaka. Alikuwa mwepesi wa kuanzisha mashambulizi anapoona timu imekaa katika mwelekeo wa kushambulia. Kwa ujumla alifanya kazi nzuri.
Beki wa kulia, Erasto Nyoni pamoja na kukosa penalti dakika ya 25, lakini bado alifanya kazi nzuri. Alikuwa anazuia na kupanda mno kusaidia mashambulizi.
Nyoni alikuwa akiipeleka mno timu mbele na kutia krosi. Alikutana kizingiti, beki wa Tottenham Hotspur ya England, Assou Ekotto lakini alipambana na mara kadhaa alifanikiwa kupiga krosi dhidi yake.
Beki wa kushoto, Shomary Kapombe naye alifanya kazi nzuri ya kuzuia na kusaidia mashambulizi.
Alikuwa akipanda kusaidia mashambulizi na kutoa pasi na krosi nzuri kwa washambuliaji, Mrisho Ngassa na Mbwana Samatta.
Kuna wakati Kapombe alijaribu kuingia mwenyewe kwenye eneo la hatari na kwa ujumla alionyesha ni mchezaji mwenye mustakabali mzuri katika timu ya taifa.
Mabeki wa kati, Aggrey Morris na Kevin Yondan hao ndio wanastahili pongezi kubwa sana kwa kutulia na kucheza kwa uelewano mkubwa.
Hakika waliweza kumlinda vema kipa wao, dhidi ya washambuliaji hatari, wenye kila kitu na dakika 90 zikamalizika bila ya nyavu za Stars kuguswa.
SAFU YA KIUNGO:
Jambo la kufurahisha zaidi, mbele ya walinzi siku hiyo walikuwa wakicheza viungo wawili, Frank Domayo na Salum Abubakar 'Sure Boy' kama viungo wa ulinzi, ambao walifanya kazi nzuri mno.
Walikuwa wakisaidia mno ukabaji, na wakati huo huo wakiipandisha timu kwa haraka wakishirikiana na viungo wenzao Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba, ambao walikuwa wachezeshaji jana.
Mfumo wa sasa Stars ni sehemu nyingine ya burudani, iliyobeba matumaini ya timu ya taifa, kucheza kitimu na kwa uelewano wa hali ya juu.
Uchezaji wa aina ile, wa kila mchezaji kuwajibika uwanjani, timu inapokuwa ina au haina mpira ndiyo ya maana ya nidhamu ya kiuchezaji na kama timu itaendelea hivyo, kuna uwezekano wa ndoto kutimia.
Viungo hawa wote walikuwa wakichezesha timu na wote walikuwa wakikaba na hilo lilisaidia sana Stars Jumatano kutoingia kwenye makucha ya Simba Wasiofungika.
Pasi muruwa walizokuwa wakipiga zilikuwa mtihani mzito kwa wachezaji wa Cameroon, ambao pamoja na kujitahidi kuibana Stars kwa dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili walichemsha.
Walichemsha na kuwaacha vijana wa Tanzania wakiwarusha mashabiki wao kwa shangwe za burudani ya kandanda safi yenye kupendeza.
SAFU YA USHAMBULIAJI:
Ukweli usiopingika, Cameroon ina ukuta imara sana ukiongozwa na mkongwe, beki wa zamani wa Fulham ya England, Pierre Wome.
Mabeki wa Cameroon wanacheza vizuri mno, kwa umakini wa hali ya juu na mbaya zaidi wanajulia mno mitego ya kuotea na hiyo iliwasumbua sana washambuliaji wa Stars siku hiyo, haswa Mbwana Samatta.
Mrsiho Ngassa kwa kuwa alikuwa anaombea mipira kwa nyuma kidogo aingie nayo kwenye eneo la hatari, yeye hakukumbana na adha ya kutegeshewa mitego ya kuotea, zaidi ya kudhibitiwa vikali na Ekotto.
Ekotto alifanikiwa kuinasa mipira mingi ya Ngassa na kwa ujumla siku hiyo nyota huyo wa Simba SC, alifichwa.
Lakini bado wachezaji wa Stars waliendelea kupambana kuhakikisha kipyenga cha kuhitimisha mchezo hakilii kabla hawajapata bao.
Na kweli, walifanikiwa kupata bao wakati baadhi ya mashabiki wamekwishaanza kuachia siti zao.
Samatta siku hiyo ndiye mshambuliaji aliyefanikiwa kuichachafya zaidi ngome ya Cameroon na hata penalti ambayo Stars waliipata, ilitokana na pilika zake.
BENCHI LA UFUNDI:
Mabadiliko yaliyofanywa na Stars siku hiyo, kumtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza mshambuliaji Thomas Ulimwengu kwa kiasi kikubwa yalichangia kupatikana kwa bao hilo pekee la ushindi.
Ilionekana ni mipango, ambayo kocha Mdenmark Kim Poulsen na wasaidizi wake, Sylvester Marsh na Juma Pondamali waliingia nayo uwanjani.
Kwanza, kulundika viungo wengi ili wakazibe njia za Cameroon kuipitisha mipira, lakini baadaye kabisa, kupunguza kiungo na kuongeza mshambuliaji, ili kuzidisha nguvu ya mashambulizi na hatimaye kupatikana kwa japo bao kama si mabao.
Ilikuwa kazi nyepesi kwa mabeki wa Cameroon kumuwekea mtego wa kuotea mshambuliaji mmoja wa Stars, Samatta ambaye baadaye akawa analazimika kuchezea pembeni zaidi.
Lakini baada ya kuingia Thomas Ulimwengu, mabeki wa Cameroon wakajikuta wana majukumu ya kudhibiti washambuliaji wawili.
Wakati huo huo, Ngassa alikuwa anahama hama kutoka upande mmoja wa Uwanja hadi mwingine kutafuta nafasi, kwa hiyo dakika takriban 10 za mwishoni, Cameroon walielemewa.
Na Stars haikuwa ikishambulia kutokea upande mmoja tu kama ilivyozoeleka au jinsi ambayo timu zetu nyingi nchini hufanya, siku hiyo ilikuwa ikishambulia kutokea pande zote.
Kwa sababu hiyo, mabeki wa Cameroon walikuwa wana kazi mno ya kumulika pande zote mbili hizo, kushoto na kulia na bado wakati mwingine zilikuwa zinapenyezwa pasi katikati.
STARS INATIA MATUMAINI:
Kwa ujumla Stars imebadilika kwa kiasi kikubwa, Jumatano ikishinda mechi ya tatu kati ya nne ilizocheza ndani ya miezi minne iliyopita.
Novemba, iliifuna Kenya 1-0 mjini Mwanza, Desemba ikaifunga Zambia 1-0 mjini Dar es Salaam na Januari ikafungwa 2-1 ugenini nchini Ethiopia.
Bila shaka, kocha Poulsen na wasaidizi wake sasa kuelekea mechi dhidi ya Morocco wamepata mwanga mzuri na sasa kuna matumaini makubwa ya kuchukua pointi tatu mwezi ujao mikononi mwa Waarabu hao. Kila la heri Taifa Stars katika kampeni za kuwania tiketi ya Kombe la Dunia Brazil 2014 na shukrani kwao wadhamini wa timu yetu, Kilimanjaro Premium Lager kwa kufanikisha maandalizi mazuri kama haya.