• HABARI MPYA

    Sunday, April 07, 2013

    KUTAFUTA ‘E PLURIBUS UNUM!

    NILISHANGAZWA sana na maoni mbalimbali niliyoyapata kuhusiana na safu hii wiki iliyopita. Imenipa nguvu sana kuendelea kuandika. Namshukuru sana Bin Zubeiry kwa kutupa blogu hii na sehemu ya kusemea.

    Tunaendelea sasa.
    SIKUMBUKI vizuri lakini nadhani alikuwa ni mwanafalsafa maarufu wa Uyunani, Heraclatus, ambaye aliibuka na neno hili; E Pluribus Unum. Unaweza kutafsiri kwa maana kubwa mbili, moja ukasema Mmoja Kutoka Katika Wengi au Katika Wengi, Mmoja.
    Unaweza kutoa mfano wa Marekani kutoka katika maana hii. Majimbo zaidi ya 50 yakaungana kuunda taifa moja la Marekani. Kutoka katika majimbo hayo mengi, ikaibuka Marekani.
    Lakini kuna maana ya pili, Waingereza wanasema A Defining Moment. Kuna jambo linalotokea katika historia ya nchi, eneo au mtu binafsi ambalo linabadilisha kabisa historia ya kitu hicho.
    Kila mtu, kila taifa na karibu mambo mengi yana wasaa huu. E Pluribus Unum, wanasema Walatini. Wasaa ambao mtu mdogo anakuwa amekua. Wasaa ambao taifa dogo linakuwa taifa kubwa. Narudia, E Pluribus Unum.

    Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu Tanzania

    BADO napitia nakala yangu ya Mpango wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania uliozinduliwa katikati ya wiki hii jijini Dar es Salaam.
    Najua, wapo watu ambao wataibuka na kutaja ‘matobo’ yaliyomo katika mpango huo. Kwa bahati nzuri, walioandaa mpango huo tayari wametangaza kwamba watapokea maoni yoyote ya kuboresha mpango huo.
    Furaha yangu ni kwamba walau sasa tumeandaa mpango wetu wenyewe wa kuendeleza soka letu. Tuna bahati kwamba tuna mtu kama Henry Tandau ambaye alisomeshwa na taifa letu kusaidia michezo na amefanya makubwa kwenye kuandaa mpango huu.
    Kwa muda mrefu, mchezo wa soka uliendeshwa bila ya dira. Katika klabu ya Simba, ndiyo kwanza sekretarieti inapambana kuhakikisha klabu inaendeshwa na dira ambayo kiongozi yeyote atakayeongoza Simba huko mbele ya safari ataifuata.
    Bila ya dira hakuna mwelekeo. Ndiyo maana mpango huu una maana kubwa sana kwa yeyote yule mwenye nia njema na klabu. Ni vema wale wenye michango ya kuboresha mpango huu wakaitoa ili tuboreshe.
    Sina uhakika sana lakini nadhani mpango huu unaweza kuwa E Pluribus Unum kwenye sekta ya soka Tanzania. Pengine, huu ndiyo wakati ambapo soka la Tanzania litahama kutoka kuwa dogo na kuwa kubwa, kubwa sana walau kwa hapa Afrika.

    Jina, Jina, Jina…… Lina nini?

    HIVI karibuni, nimesoma kwenye vyombo vya habari kuhusu kijana mmoja wa mkoa wa Mbeya anayetaka kulipwa fidia na Omega Seme wa Yanga kwa sababu ametumia jina lake kupata umaarufu.
    Kijana huyo anadai kwamba jina hilo la Omega Seme ni la kwake na kwamba anayetumia jina hilo kwa sasa (mchezaji wa Yanga) alilipata kwa njia zisizo halali.
    Stori iko hivi.. Kijana huyo anadai kwamba aliwahi kuteuliwa kujiunga na timu ya vijana ambayo baadaye ilikuja kuwa timu ya taifa ya vijana ya Tanzania.
    Jina lake lilikuwa miongoni mwa walioteuliwa lakini badala ya kupelekwa yeye, akapelekwa Omega wa Yanga kwa kutumia jina lake.
    Omega huyo wa Yanga akapata nafasi kwenye timu ya taifa. Pengine, fursa hiyo ya kujiunga na Ngorongoro Heroes ilikuwa E Pluribus Unum kwake. Aliihitaji na ikajitokeza.
    Sasa swali linakuja, Seme alipata nafasi ya kusajiliwa na Yanga kwa sababu ya jina au kwa sababu ya uwezo wake? Jibu langu ni rahisi sana, uwezo wake.
    Naweza nikapata mtoto wa kiume leo na nikamwita Diego Maradona. Je, atakuja kuwa na uwezo kama Mu-Argentina huyo? Au ukimwita Jakaya Kikwete naye atakuja kuwa Rais wa Tanzania?
    Mawazo yangu ni kwamba jina si kitu. Mahmoud Zubeirry amekuwa alivyo sasa kutokana na malezi aliyopata, makuzi yake, mazingira aliyokulia, watu aliokutana na kipaji fulani alichopewa na mwenyezi Mungu.
    Unahitaji E Pluribus Unum kwenye sehemu moja katika maisha yako ili uweze kuwa mtu tofauti. Nilipata nafasi ya kusoma Agricultural Economics katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) lakini sikwenda na nikachagua Uandishi wa Habari.
    Kwangu, hiyo ndiyo ilikuwa E Pluribus Unum kwenye maisha yangu. Mambo yote ninayofanya sasa yametokana na maamuzi yangu ya wakati huo. 
    Bill Gates aliacha masomo chuo kikuu na kuanza shughuli zake binafsi na leo ndiyo tajiri namba moja duniani. Angeendelea na masomo pengine leo angekuwa profesa mmoja wa chuo kikuu Marekani mwenye fedha za kawaida tu.
    Kuna habari kuhusu Waziri mmoja wa serikali ya Kikwete ambaye anadaiwa kutumia majina mbalimbali kufika alipo sasa. Hakuna miongoni mwa aliotumia majina yao aliyewahi kulalamika.
    Amefika hapo alipo sasa kwa sababu ya juhudi zake mwenyewe na ujanja. Kuna jina moja alilotumia wakati mmoja ndilo likaja kuwa E Pluribus Unum kwake. Asingefanya hivyo, asingekuwa hapo alipo kwa sasa.
    Jina halina kitu chochote cha maana ndani yake. Unaweza kuitwa Aristotle Socrates Gates Slim na bado ukaishia kuwa ombaomba mitaani lakini mzaliwa mmoja wa Iramba anayeitwa Tundu Lissu, akaibuka kuwa bonge la tajiri.
    Tumwache Omega Seme acheze mpira wake.

    Aaah, sijatumia maana moja
    NAJUA mtakuwa mnajiuliza natumiaje maana nyingine ya E Pluribus Unum. Hebu angalia kuna blogu ngapi hapa nchini? Kumi, 20 au 30… Sijui.
    Katika zote hizo, nimetumia hii ya Bin Zubeirry kuandikia safu hii ya Ordem E Progresso… Hivyo, Bongostaz.blogspot ni E Pluribus Unum kwangu, katika blogu nyingi, nimeteua hii moja. Mpaka wikiendi ijayo

    KUNRADHI: Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu, safu imechelewa kuwajia jana na badala yake imekuja leo. Lakini ratiba inabaki kuwa vile vile, kila Jumamosi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KUTAFUTA ‘E PLURIBUS UNUM! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top