• HABARI MPYA

    Monday, April 08, 2013

    PRIMO NDIYE OFISA WA FIFA ANAYEKUJA KUTATUA MGOGORO WA UCHAGUZI TFF, AZUNGUMZA NA BIN ZUBEIRY NA KUTHIBITISHA UJIO WAKE WIKI IJAYO

    Anayekuja; Primo Corvaro

    Na Mahmoud Zubeiry
    MKUU wa Idara ya Vyama Wanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Primo Corvaro ndiye atakuja nchini kutatua mgogoro wa Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wiki ijayo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu leo kutoka Zurich, Usiwsi yalipo makao makuu ya FIFA, Primo amesema kwamba hana uhakika ni lini haswa atakuja Tanzania, lakini yeye ndiye anakuja kutatua mgogoro huo.
    “Ndiyo, ni mimi ninakuja, ila vyema ungezungumza na Tenga (Leodegar, Rais wa TFF) atakupa ratiba nzima,”amesema Primo.   
    Tayari TFF imekwishasema msafara wa FIFA utashughulikia mgogoro huo kwa siku mbili nchini, Aprili 16 na 17 mwaka huu.
    Kwa mujibu wa utaratibu wa kesi kama hizi, Primo anaweza kuambatana na mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Vyama Wanachama wa FIFA na Ofisa Maendeleo wa Kanda hii, Ashford Mamelodi.
    Wajumbe wa Afrika waliomo ndani ya Kamati hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti, Mturuki Fenes Erzik ni Leodegar Tenga wa Tanzania, Kwesi Nyantakyi wa Ghana, Mohamed Raouraoua wa Algeria ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Walter Nyamilandu wa Malawi, Adam Mthethwa wa Swaziland na Amidou Djibrilla wa Niger.
    Hivi karibuni wakati wa mgogoro wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Primo aliongozana na Mamelodi na Tenga mjini Kampala. Kwa kuwa Tenga ni sehemu ya mgogoro huu, Primo anaweza kuongozana na Mjumbe mwingine yeyote kutoka Wajumbe hao wa Afrika.  
    Primo kulia, akiwa na Ashford Mamelodi katikati na Ofisa Mtendaji Mkuu wa FUFA, Edgar Watson hivi karibuni nchini Uganda

    TFF inakabiliwa na mgogoro wa uchaguzi, baada Kamati ya Rufaa ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola kuwaengua mgombea Urais, Jamal Malinzi katika mazingira ya mizengwe na kumuacha Makamu wa sasa wa kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee katika nafasi ya Urais.
    Malinzi alikata rufaa FIFA na uchaguzi ukasimamishwa hadi suala hilo lichunguzwe. Katikati ya sakata hilo, Serikali nayo ikasimamisha Katiba mpya ya TFF iliyopitishwa mwaka jana kwa njia ya waraka, kwa sababu ni kinyume cha katiba ya mwaka 2006 na kuagiza iitishe Mkutano Mkuu kupitisha Katiba mpya kwa mwongozo wa Katiba iliyopo mezani.
    Hata hivyo, baadaye pande hizo mbili, Serikali na TFF ziliketi meza moja na kufikia makubaliano ya kuwaacha kwanza FIFA waje kutatua mgogoro wa uchaguzi ndipo masuala mengine yataendelea.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: PRIMO NDIYE OFISA WA FIFA ANAYEKUJA KUTATUA MGOGORO WA UCHAGUZI TFF, AZUNGUMZA NA BIN ZUBEIRY NA KUTHIBITISHA UJIO WAKE WIKI IJAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top