![]() |
| Jerry Tegete |
Na Mahmoud Zubeiry
KUKOSA mabao ni suala moja kwa safu ya ushambuliaji ya vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC na sasa balaa lingine linaanza kuinyemelea safu hiyo, ambalo ni la majeruhi.
Tayari mshambuliaji mzoefu wa kwafunga wapinzani wa jadi, Simba SC, Jerry Tegete yupo kitandani hivi sasa akitibiwa goti aliloumia wiki iliyopita.
Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Tegete aliumia siku chache kabla ya Yanga kwenda kumenyana na Polisi Morogoro na hadi leo ameshindwa kuanza mazoezi.
“Yuko chini ya uangalizi wa Daktari (Nassor Matuzya), tutajua zaidi kutoka kwake baadaye,”alisema Kizuguto.
Mbali na Tegete, wachezaji wengine wa Yanga ambao hawafanyi mazoezi kwa sasa ni beki Ladislaus Mbogo aliyefanyiwa upasuaji wa uvimbe wa shavu na kiungo Omega Seme anayesumbuliwa na nyama za paja.
Wakati huo huo: Kikosi cha Yanga leo kimerejea kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam badala ya Mabatini Kijitonyama.
“Tumerudi Loyola, tulihama pale kwa sababu walikuwa wanakarabati, ila kwa sasa wamekamilisha na timu imerudi pale ambako angalau Uwanja wao ni mzuri,”amesema Kizuguto.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na JKT Oljoro katika mfululizo wa Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa kileleni kwa pointi zake 49, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 43, Kagera Sugar 37 na mabingwa watetezi Simba 35.
Lakini katika siku za karibuni, safu ya ushambuliaji ya Yanga inaonekana kupoteza makali, ikiwa imevuna mabao manne tu katika mechi tano zilizopita, dhidi ya Ruvu Shooting, Azam FC, Kagera Sugar, Toto African na Polisi Morogoro.
Na katika mabao hayo manne, matatu yamefungwa na viungo, Haruna Niyonzima mawili dhidi ya Azam na Kagera na Nizar Khalfan dhidi ya Ruvu Shooting, wakati lingine ndiyo lilifungwa na mshambuliaji Hamisi Kiiza dhidi ya Toto.



.png)