• HABARI MPYA

    Tuesday, May 07, 2013

    BOCCO HALI BADO TETE...AZAM YATUA DAR, LAKINI AKILI YAKE YABAKI PRINCE MOULAY

    Cheki sura hiyo; John Bocco 'Adebayor' jana kwenye ndege

    Na Mahmoud Zubeiry
    AZAM FC imetua jana jioni Dar es Salaam, ikitokea Morocco ambako imetolewa katika Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hali ya mshambuliaji wake John Raphael Bocco ‘Adebayor’ bado si nzuri.
    Tofauti na ilivyo kawaida yake, Bocco ni mcheshi mbele ya wenzake, lakini tangu anaondoka hoteli ya Golden Tulip, Rabat juzi hadi anafika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam jana jioni alikuwa mnyonge sana.
    Muda wote alikuwa amelala kwenye ndege na hata wahudumu walipomuamsha kwa ajili ya chakula, Bocco hakutaka na alikuwa mkali.  Angalau David Mwantika anaonekana kukubaliana na hali halisi na alionekana kidogo kuwa katika hali ya kawaida kwenye ndege wakati wa kurejea Dar es Salaam.
    Bocco kushoto

    Wachezaji wote hao wawili wa Azam, beki Mwantika ‘Bedui’ na Bocco ‘Adebayor’ wako katika hali mbaya na kutokana na kusononeka kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa timu yao kutolewa na AS FAR Rabat katika Kombe la Shirikisho.   
    Azam Jumamosi ilifungwa mabao 2-1 na Rabat kwenye kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah na wenyeji AS FAR Rabat na kutolewa katika Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Mwantika aliidhoofisha Azam siku hiyo kwa kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 56 kwa kumchezea rafu mchezaji wa Rabat na pia alisababisha penalti iliyowapa bao la kwanza Rabat dakika ya 12 ambalo lilikuwa la kusawazisha, baada ya Bocco kutangulia kufunga dakika ya sita.
    Kwa ujumla, Mwantika siku hiyo hakuwa katika ubora wake- kwani hata faulo alizocheza na kusababisha penalti ilikuwa ‘si ya lazima’ na hata kadi nyekundu pia angeweza kuiepuka kama asingemsukuma hadi kwenye lami mchezaji wa Rabat.   
    Azam ilihitaji sare yoyote ya mabao ifuzu na ilikaribia kuipata dakika ya 81 ilipopata penalti ikiwa nyuma kwa mabao 2-1, lakini fundi wa upigaji wa michomo hiyo, John Raphael Bocco alikwenda kugongesha mwamba wa juu mpira huo.
    Kipre Tchetche kushoto

    Meneja Patrick Kahemele...

    Karim Mapesa akimtazama Nassor ...
    Dakika ya 88, kona nzuri iliyochongwa na Khamis Mcha ‘Vialli’ iliunganishwa vizuri kwa kichwa na Bocco, lakini beki mmoja wa Rabat akaiwahi kwenye chaki na kuiondosha kwenye eneo la hatari.
    Azam FC iliondoka juzi asubuhi mjini Rabat saa 4:00 kwa basi kwa saa za huko na saa 6:00 kwa saa za Tanzania kwenda Casablanca kuunganisha ndege hadi Dubai, ambako ililala na kuondoka na asubuhi ya jana moja kwa moja kurejea Dar es Salaam.
    Azam ilisafiri kwa saa mbili hadi Cassablanca ambako ilipanda ndege ya shirika la Emirates, wadhamini wa Arsenal ya England kwa saa tisa hadi Dubai na jana ikatumia saa sita kutoka Dubai hadi Dar es Salaam, ambako ilifika jioni. 
    Pamoja na uchovu wa safari, Azam watacheza na Mgambo JKT Jumamosi katika Ligi Kuu, Uwanja wa Chamazi mchezo ambao wanatakiwa lazima washinde ili kujihakikishia tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani tena.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BOCCO HALI BADO TETE...AZAM YATUA DAR, LAKINI AKILI YAKE YABAKI PRINCE MOULAY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top