• HABARI MPYA

    Tuesday, May 07, 2013

    KHAMIS MCHA VIALLI: SAMATTA HABEBI TUZO MBELE YANGU

    Mcha akichuana na beki wa AS FAR Rabat Jumamosi

    Na Mahmoud Zubeiry
    KHAMIS Mcha ‘Vialli’ ni miongoni mwa wachezaji walioingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora katika tuzo za wanamichezo Bora wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), akichuana na akina John Bocco ‘Adebayor’ anayecheza naye Azam FC, Kevin Yondan wa Yanga SC, Shomary Kapombe wa Simba, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, wote wa TP Mazembe ya DRC.
    Mcha ni kati ya wachezaji wanaofanya vizuri Tanzania hivi sasa na katika mahojiano na BIN ZUBEIRY jana Dubai, UAE akiwa njiani na klabu kurejea Tanzania wakitokea Morocco, ambako walikwenda kucheza na AS FAR Rabat, kijana huyo alisema mengi. Endelea.
      
    Vialli wa Azam

    BIN ZUBEIRY: Salaam alaykum Vialli.
    MCHA: Waalaykum Salam kaka Bin Zubeiry.
    BIN ZUBEIRY: Kwanza niambie, unajisikiaje kuingia kwenye kunyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora Tanzania?
    MCHA: Nafurahi sana kwa kweli, kwani hii ni nafasi ya kipekee kwangu.
    BIN ZUBEIRY: Kati yenu mlioingia kwenye tuzo hii, nani anastahili kushinda unadhani?
    MCHA: Mimi
    BIN ZUBEIRY: Kwa nini?
    MCHA: Nimefanya vizuri mwaka jana, tena sana tu. Nimepata mafanikio na timu yangu ya taifa ya Zanzibar nikiiwezesha kushika nafasi ya tatu katika Kombe la Challenge kule Uganda, tena tuliwafunga hao hao Bara ambao ndio nimeingia nao kwenye kuwania tuzo, mimi nikiwa Mzanzibari pekee. Lakini pia nimekuwa na msimu mzuri na klabu yangu Azam FC. Nimeiwezesha kushika nafasi ya pili na kucheza michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza mwaka huu. Tumekuwa washindi wa pili wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati (Kagame). Tumechukua Kombe la Mapinduzi. Kwa kweli mimi haswa ndiye nastahili hii tuzo.  
    BIN ZUBEIRY: Desemba mwaka uliitwa kwa mara ya kwanza Taifa Stars, lakini hivi karibuni umehamishiwa kikosi cha pili (Young Taifa Stars), umeipokeaje hiyo? 
    MCHA: Nimeipokea kwa uzuri tu, ni mipango ya kocha na yeye ndiye anajua mimi nastahili kuwa wapi na kwa sababu gani.
    BIN ZUBEIRY: Unasemaje kuhusu kutolewa kwenu Kombe la shirikisho? 
    MCHA: Ni kawaida ya mchezo, inatokea katika soka. Mechi ya kushinda inatokea mnafungwa. Imeniumiza, lakini ndiyo soka.
    BIN ZUBEIRY: Ulikuwa katika hali gani refa alipowapa penalti ambayo mngefunga mngefuzu? 
    MCHA: Nilipata nguvu na msisimko wa hali ya juu. Kutokana na mechi ilivyokuwa ikienda, sikutegemea kwa kweli kama refa angetoa penalti kama ile. Nilipata nguvu za ajabu sana.
    BIN ZUBEIRY: Bila shaka ulimuamini mpigaji
    MCHA: Ndiyo, kwa asilimia 100
    BIN ZUBEIRY: Na ilipogonga mwamba ulikuwaje?
    MCHA: Nilikuwa nimejiandaa kushangilia kwa kujua kapteni anafunga. Ilipogonga mwamba, nilipigwa butwaa. Ila ikabidi tu nirudi mchezoni tutafute nafasi nyignine. 
    BIN ZUBEIRY: Wewe ni mpigaji mzuri wa penalti na Ilipotokea penalti ulikuwepo pale mbele ukachukua mpira na kumpelekea Bocco. Kwa nini hukutaka kupiga wewe?
    MCHA: Mimi nilichukua mpira nikampa Kapteni, yeye kama angeona hawezi kupiga angempa mtu mwingine. Lakini akapiga.
    BIN ZUBEIRY: Hii ni mara ya ngapi unacheza michuano ya Afrika?
    MCHA: Mara ya tatu
    BIN ZUBEIRY: Mara ya kwanza?
    MCHA: Nikiwa na Miembeni mwaka 2009 tulicheza na timu ya Zimbabwe tukatolewa Raundi ya Kwanza 
    BIN ZUBEIRY:  Mara ya pili?
    MCHA: Nikiwa na Ocean View tukatolewa na timu ya DRC.
    BIN ZUBEIRY: Kwa hivyo wewe ni mchezaji mzofu wa michuano mikubwa hivi sasa?
    MCHA: Ndiyo
    BIN ZUBEIRY: Umegundua tofauti gani kati ya soka yetu na wenzetu?
    MCHA: Tofauti ndogo ndogo sana, kuna nchi zinatuzidi na kuna nchi tunazididi.
    BIN ZUBEIRY: Azam mwakani mnaweza kurudi tena kwenye michuano ya Afrika, je mtavuka hatua mliyokwamia?
    MCHA: Tunatarajia hivyo, kwa sababu kutolewa kwa mwaka huu imekuwa chachu kwetu. Mwakani tutafanya vizuri zaidi.
    BIN ZUBEIRY: Huu ni msimu wako wa pili Azam, umebakiza muda gani kumaliza mkataba?
    MCHA: Napenda mkataba wangu uwe siri na mwajiri wangu.
    BIN ZUBEIRY: Wewe ni mchezaji mzuri, na kila timu inataka mchezaji mzuri, ikitokea timu ambayo ni mpinzani wa Azam kama Simba au Yanga ikakutaka, utakubali ofa?
    MCHA: Itategemea na timu yangu. Ikitokea ofa nitawaambia viongozi wangu. Wakikubali niondoke nitakwenda, wasipokubali nitabaki. Maisha ya mpira hayatabidiliki. Siwezi mimi kusema sitacheza Simba na Yanga. Inaweza kutokea Azam wenyewe wakaamua niende huko.
    BIN ZUBEIRY: Mchezaji gani anakuvutia Tanzania?
    MCHA: Yule mtu mfupi wa Azam
    BIN ZUBEIRY: Ndiyo nani?
    MCHA: Sure Boy (Salum Abubakar)
    BIN ZUBEIRY: Kwa nini?
    MCHA: Kwa staili ya uchezaji wake. Naipenda sana.
    BIN ZUBEIRY: Kwa duniani?
    MCHA: Messi
    BIN ZUBEIRY: Na unapenda timu gani duniani? 
    MCHA: Chelsea
    BIN ZUBEIRY: Soka ni mchezo ambao wewe unafuata nyayo kwenye ukoo wenu, au wewe ndiyo unaanza?
    MCHA: Nafuata nyayo za baba. Alicheza KMKM, Miembeni alikuwa maarufu kwa jina la Mcha Khamis, yeye alikuwa winga kama mimi na mshambuliaji. Hata mama (Wahida Seif) alicheza Netiboli JKU, Bandari na timu ya taifa Zanzibar.
    BIN ZUBEIRY: Hili jina la Vialli limetoka wapi?
    MCHA: Limetokana na rafiki yangu mmoja (Shomary) wakati nikiwa mdogo, nilikuwa napenda sana kunyoa vipara. Ndiyo akaanza kuniita Vialli. Ndiyo imekuwa Vialli hadi leo. 
    BIN ZUBEIRY: Soka ya Afrika ni sehemu ya kuanzia, wachezaji wengi wanaota kucheza Ulaya, vipi kwa upande wako ukiwa na umri wa miaka 24 sasa?
    MCHA: Hata mimi ni hivyo hivyo, nategemea Mungu akijaalia nicheze Ulaya.
    BIN ZUBEIRY: Umewahi kupata ofa yoyote tangu uanze kucheza soka?
    MCHA: Bado
    BIN ZUBEIRY: Ulijiunga na Azam ukitokea gani na mwaka gani?
    MCHA: Niliingia Azam mwaka 2011 nikitokea Ocean View. 
    BIN ZUBEIRY: Mbali na Ocean View, timu gani nyingine umechezea?
    MCHA: Miembeni na timu ndogo ndogo za watoto zilizonikuza kama Kwahani, Mbuyuni na Town Boys.
    BIN ZUBEIRY: Unawaambia nini wapenzi wenye tabia ya kuzomea timu ikifanya vibaya?
    MCHA: Nawaambia wabadilike, wawe tayari kupokea matokeo yote na waiunge mkono timu yao siku zote.
    BIN ZUBEIRY:  Umeoa, au una watoto tayari?
    MCHA: Bado
    BIN ZUBEIRY: Kwa nini?
    MCHA: Muda bado, wakati ukifika nitaoa inshaallah. Kwa sasa akili yangu ipo kwenye soka kwanza.
    BIN ZUBEIRY: Nashukuru Vialli?
    MCHA: Asante Bin Zubeiry, nimefurahi sana kufanya mahojiano na wewe.
    BIN ZUBEIRY: Asante, nipo kwa ajili yenu sheikh. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KHAMIS MCHA VIALLI: SAMATTA HABEBI TUZO MBELE YANGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top