![]() |
Isha Mashauzi anawania tuzo ya Msanii Bora wa Kike Taarabu |
ZOEZI la upigaji wa kura za tuzo za wanamuziki bora Tanzania, maarufu kama Kilimanjaro Music Award lililoanza Mei 2, mwaka huu linazidi kupamba moto kwa wapenzi wa muziki kuwapigia kura wasanii wawapendao.
Jana kwa muhtasari tulielezea ushindani uliopo katika kipengele cha Msanii Bora wa Kike na wa Kiume. Msanii Bora wa Kiume washindani ni Ben Pol, Diamond, Linex, Mzee Yussuf na Ommy Dimpoz kwa ‘wakaka’, wakati Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Lady Jaydee, Mwasiti na Recho watawania tuzo ya Msanii Bora wa Kike.
![]() |
Mzee Yussuf, anawania Msanii Bora wa Kiume Taarab |
Ikumbukwe tulianza uchambuzi wetu kwa kutazama kipengele cha wimbo bora wa mwaka ambapo Rapa Kala Jeremiah, kupitia wimbo wake Dear God anachuana na kundi la Kigoma All Stars na wimbo wao Leka Dutigite, Mwasiti aliyemshirikisha Ally Nipishe katika wimbo Mapito, Ommy Dimpoz aliyemshirikisha Vanessa Mdee katika wimbo Me n U na Ben Pol katika wimbo Pete.
Leo, tunahamia katika vipengele vya Msanii Bora wa Kike Taarab na wa Kiume. Kwa wanawake, washindani ni Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Khadija Yussuf na Leila Rashid, wakati tuzo ya Msanii Bora wa Kiume ya muziki huo wa mwambao itawaniwa na Ahmed Mgeni, Hashim Said na Mzee Yussuf.
Wasanii wote walioingia kuwania tuzo hizo ni ambao kwa hakika mwaka jana walitamba katika medani ya muziki nchini. Ni wasanii wanaobeba maana halisi ya Usanii bora- kutokana na kazi na wajihi wao.
Hakika kuna ushindani mkubwa katika vipengele hivi na zaidi msanii atabebwa na idadi ya kura atakazopigiwa na mashabiki wake ili aweze kushinda tuzo hiyo.
Wapiga kura wanatakiwa kuandika namba ya msanii, wimbo, kikundi au bendi anayotaka ishinde na kisha kutuma kwenda namba 15346, wakati njia nyingine zaidi ya ujumbe mfupi (SMS) ni pamoja na Email, kwenda ktma@innovex.co.tz au kutembelea tovuti ya www.kilitimetz.com na kupiga kura moja kwa moja.
Meneja wa Bia Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba, wamejiandaa vizuri mwaka huu kuhakikisha zoezi linafana.
Kilele cha sherehe za utoaji tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards zilizobeba kaulimbiu ya Kikwetu kwetu ni Juni 8, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, ambako pamoja na wasanii mbalimbali kupokea tuzo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali pia.
Je, katika Msanii Bora wa Kike na wa Kiume wa Taarab, utampa nani na nani kura zako?