![]() |
Profesa Jay kulia na Fid Q kushoto miongoni mwa wanaowania tuzo |
Na Princess Asia, IMEWEKWA MEI 14, 2013 SAA 5:31 ASUBUHI
ZOEZI la upigaji wa kura za tuzo za wanamuziki bora Tanzania, maarufu kama Kilimanjaro Music Award lililoanza Mei 2, mwaka huu linazidi kupamba moto kwa wapenzi wa muziki kuwapigia kura wasanii wawapendao.
Jana kwa muhtasari tulielezea ushindani uliopo katika vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa kike wa Bendi, ambako Kwa wananaume, Chaz Baba anachuana na Dogo Rama, Greyson Semsekwa, Jose Mara na Khaleed Chokora na kwa wanawake Anneth Kushaba anachuana na Luiza Mbutu, Mary Lucos na Vumilia.
Awali tulitazama vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa Kike Bongo Fleva, ambako kwa wanaume, Ally Kiba anachuana na Ben Pol, Diamond, Linex na Ommy Dimpoz, wakati kwa wanawake Linah anapambana na Mwasiti, Recho na Shaa.
Tulitazana pia vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa Kike Taarabu, ambako Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Khadija Yussuf na Leila Rashid wanawania Umalkia na akina Ahmed Mgeni, Hashim Said na Mzee Yussuf wanapigania Ufalme.
Kabla ya hapo, tulitazama vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa Kike kwa ujumla, ambavyo vinawashindanisha Ben Pol, Diamond, Linex, Mzee Yussuf na Ommy Dimpoz kwa ‘wakaka’, wakati Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Lady Jaydee, Mwasiti na Recho watawania tuzo ya Msanii Bora wa Kike.
Ikumbukwe tulianza na kutazama kipengele cha wimbo bora wa mwaka ambako Rapa Kala Jeremiah, kupitia wimbo wake Dear God anachuana na kundi la Kigoma All Stars na wimbo wao Leka Dutigite, Mwasiti aliyemshirikisha Ally Nipishe katika wimbo Mapito, Ommy Dimpoz aliyemshirikisha Vanessa Mdee katika wimbo Me n U na Ben Pol katika wimbo Pete.
Leo tunahamia kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Hip hop ambacho kinawashindanisha Fid Q, Joh Makini, Kala Jeremiah, Profesa Jay na Stamina.
Hakika hapa shughuli ipo, Hip hop ni muziki wa aina yake na ukiuchukulia kijuu juu unaweza kupoteza kura yako. Inatakiwa kutulia kwa umakini na kurudia mara mbili mbili kumtathmini msanii kabla ya kutoa kura yako, ili kuhakikisha unampa mtu anayestahili kushinda.
Pamoja na yote, wasanii wote walioingia kuwania tuzo hii ni wakali na mwaka jana walitamba katika medani ya muziki nchini.
Hakika kuna ushindani mkubwa katika kipengele hiki na zaidi msanii atabebwa na idadi ya kura atakazopigiwa na mashabiki wake ili aweze kushinda tuzo hiyo.
Wapiga kura wanatakiwa kuandika namba ya msanii, wimbo, kikundi au bendi anayotaka ishinde na kisha kutuma kwenda namba 15346, wakati njia nyingine zaidi ya ujumbe mfupi (SMS) ni pamoja na Email, kwenda ktma@innovex.co.tz au kutembelea tovuti ya www.kilitimetz.com na kupiga kura moja kwa moja.
Meneja wa Bia Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba, wamejiandaa vizuri mwaka huu kuhakikisha zoezi linafana.
Kilele cha sherehe za utoaji tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards zilizobeba kaulimbiu ya Kikwetu kwetu ni Juni 8, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, ambako pamoja na wasanii mbalimbali kupokea tuzo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali pia.
Je, katika Msanii Bora wa Kike na wa Kiume katika Bendi, utampa nani na nani kura zako?