IMEWEKWA MEI 12, 2013 SAA 3:00 ASUBUHI
IMEBAKI Raundi moja kukamilika kwa msimu wa 2012/2013 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Mei 18, mwaka huu zitachezwa mechi za mwisho za msimu.
Katika kalenda ya msimu huu ya matukio ya TFF, michuano ya Kombe la Taifa na FA iliorodheshwa pia mbali na Ligi Kuu, lakini yote haijafanyika pia na hadi sasa mustakabali wa michuano hiyo haueleweki.
Sote tunafahamu soka ya Tanzania ni sawa na homa za vipindi ambazo zinacheza katika kiwango fulani kwa kupanda na kushuka.
Huo ndio, ukweli na hilo linadhihirishwa na takwimu za viwango vya soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zinapotoka, Tanzania inapanda na kuporomoka, haina muendelezo wa kupanda.
Mimi si muumini sana wa takwimu hizi za FIFA, ingawa zina maana na zinatoa hali halisi, lakini mara nyingine nchi nyingine zinapanda katika staili ya maji kupwa na maji kujaa.
Katika miaka ya karibuni soka yetu ilipanda hadi tukashika nafasi ya 89, katika mwezi Desemba mwaka 2007, wakati bado Mbrazil Marcio Maximo ni kocha mkuu wa timu yetu ya taifa, Taifa Stars.
Kwa sasa chini ya Kim Poulsen soka ya Tanzania imeanza kurudi juu tena, timu yetu ya taifa inafanya vizuri katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia mwakani Brazil.
Lakini mara nyingi mambo yanapoanza kwenda vizuri kidogo katika soka ya nchi hii, hata iwe kwa bahati nasibu, wakubwa waliopewa dhamana ya kuongoza mchezo huu, hubweteka na kusahau kuhusu mipango thabiti ya kuitengenezea mihimili madhubiti soka yetu.
Sasa tunalekea wapi na kwa mtaji huu kweli tutafika, au ndiyo tutabaki kuwa watu wa kubahatisha tu miaka yote?
Tatizo letu si makocha na hata kama makocha ni tatizo kweli, ni vigumu kujua kwa sababu mfumo wetu ndio mbovu na hautoi fursa ya kuwa na wachezaji bora.
Nchi nyingi za Afrika zinabebwa na nyota wao wanaocheza Ulaya, lakini sisi tunategemea zaidi wachezaji wa nyumbani na ambao watatoka kwenye Ligi Kuu tu.
Kutoka kwenye wastani wa wachezaji 450 wanaocheza Ligi Kuu ya Bara isiyo na ushindani, inayonuka rushwa na uvundo wa uozo wa marefa wetu wasiojua, manazi na wala hongo ndio tunategemea kupata wachezaji wa kuunda timu ya taifa.
Rejea msimu uliopita, ligi yenye timu 12 maana yake kila timu ilicheza mechi 22 na bingwa akapatikana. Katika wachezaji hao 400, inawezekana nusu yake tu walicheza japo mechi 20 za msimu, wakati kitaalamu ili mchezaji awe fiti, anatakiwa kucheza mechi zisizopoungua 40 kwa msimu.
TFF pale wana Kurugenzi ya Ufundi, chini ya mwalimu aliyebobea tu Sunday Burton Kayuni ambaye sina shaka analijua hili, lakini je ametoa mwongozo utakaotuwezesha kuwa na mfumo bora na amepuuzwa au hajatoa? Wanajua wenyewe.
Rais mwenyewe wa TFF, Leodegar Chillah Tenga kitaaluma pia ni kocha na mchezaji mstaafu wa kiwango cha kimataifa, je hayajui haya?
Juzi wameibuka na tatmthiliya mpya ya Mpango Mkakati, tusubiri nayo tuone utekelezaji wake, ikiwa kalenda ya msimu tu wanashindwa kuitimiza japo kwa asilimia 50.
Tanzania tumekuwa watu wa kukariri kariri mambo, wengi sasa wanasema ‘youth’ na mashindano mengi ya vijana yameanzishwa, lakini je yanaendeshwa kwa malengo? Hapo kuna shaka.
Klabu za Ligi Kuu zimeshinikizwa kaunzisha timu za vijana na sasa ni takriban mwaka wa nne, tujiulize vipi kuhusu maendeleo ya timu hizo za vijana?
Tuna mashindano mengi ya vijana, lakini kutoka kwenye mashindano hayo mchezaji anaendelezwaje?
Nchi nyingi duniani mbali ya kuwa na Ligi Kuu, zina mashindano mengine madogo yenye msisimko kama Kombe la Ligi, Kombe la FA na Super Cup. Pia wana Ligi za vijana madhubuti, mfano pale England ligi ambayo imemkomaza kiungo chipukizi Mtanzania, Adam Nditi akiwa na Chelsea.
Uganda wana ligi hadi ya wachezaji wa akiba, ambayo imewasaidia mno kuwafanya wachezaji wao wengi wawe fiti, kwa sababu wasiocheza katika vikosi vya kwanza vya klabu zao, wanapata changamoto kupitia ligi hiyo.
Hakika mashindano haya yanaongeza msisimko wa soka katika nchi husika na wakati fulani yanafanya nchi iwe na bingwa zaidi ya mmoja.
Birmingham City ‘The Blues’ ya England waliotaka kuzuru nchini mwaka juzi kucheza na vigogo wa soka hapa nchini, Simba na Yanga, wakati huo walikuwa ni mabingwa wa Kombe la Ligi, ingawa walikuwa wamekwishaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu.
Birmingham waliifunga Arsenal katika fainali ya Kombe la Ligi mabao 2-1, Mnigeria Obafemi Martins akifunga la ushindi, msimu ambao Manchester City walitwaa ubingwa wa Kombe la FA na Man United ubingwa wa Ligi Kuu.
Hapa Tanzania, baada ya Ligi Kuu, watu wanasubiri mashindano ya ujanja ujanja tu ya watu kujitengenezea fedha, lakini hakuna tena mashindano mengine makubwa, zaidi ya hiyo michuano ya BancABC Sup8R iliyoanza mwaka jana na Simba B ikatwaa ubingwa. Labda Kombe la Mapinduzi Zanzibar.
Faida ya mashindano ya ziada kama Kombe la FA ni kutoa fursa kwa wachezaji ambao hawana namba kwenye vikosi vya kwanza nao kucheza. Kwa mfano, Kombe la FA tutarajie hadi Friends Rangers ya Manzese na Ugimbi ya Kurasini zitacheza, maana yake sasa klabu za Ligi Kuu zitaweza kutumia wachezaji wake wa vikosi vya pili, jambo ambalo litasaidia kuwakomaza.
Wakati umefika sasa, TFF ifunguke zaidi na kupanua wigo wa miundombinu ya kuinua soka ya nchi hii badala ya kuishia kufikiria tu kuwa na mashindano ya mpito pekee. Tunahitaji michuano zaidi ambayo mchezaji atacheza mechi zaidi ya 10 akionyesha umahiri ule ule.
Mifano ipo, wachezaji kama Abuu Ramadhan ‘Amokachi’, aliyewahi kucheza Yanga kabla ya mizengwe kumuondoa kwenye soka angali mdogo, alitokea kwenye mashindano ya Kombe la FA wakati bado yanafanyika nchini, akiichezea Baker Rangers ya Magomeni.
Ukweli ni kwamba Tanzania bado tuna safari ndefu kuelekea kwenye mafanikio na maana yake kazi kubwa inahitaji kufanyika, lakini ajabu TFF wanaonekana kuridhishwa na hali iliyopo.
Tazama sasa Kombe la Taifa limekufa kifo cha kawaida, kutokana na kile ambacho sisiti kusema TFF kuzidiwa ujanja au kutokuwa na mitazamo ya mbali.
Kombe la Taifa limekufa kwa sababu ya kukosa udhamini- baada ya mdhamini wake wa awali, Kampuni Bia Tanzania (TBL) iliyokuwa ikidhamini michuano hiyo kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager kuachia michuano hiyo.
Wazi, TBL walijitoa Taifa Cup baada ya kupata dili la kujitangaza kupitia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo awali ilikuwa inadhaminiwa na kampuni nyingine ya Bia nchini, Serengeti (SBL).
Haya sasa, Ligi Kuu inafikia tamati Mei 18 na mapema Katibu wa TFF, Angetile Osiah Malabeja alituambia bingwa wa Ligi Kuu atacheza Ligi ya Mabingwa na bingwa wa FA atacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Tayari tunajua kupitia Ligi Kuu, Yanga itacheza Ligi ya Mabingwa na je mwakilishi wa Kombe la Shirikisho atapatikanaje? Yangu ni hayo tu kwa leo waungwana. Nawasilisha.