![]() |
Leodegar Tenga |
Na Boniface Wambura
VYAMA vya Soka vya mikoa vimetakiwa kuendelea na mashindano ya Copa Coca-Cola yanayoshirikisha watoto wenye umri chini ya miaka 15 katika ngazi ya wilaya wakati vikisubiriwa vifaa na fedha za uendeshaji kutoka kwa mdhamini.
Wito huo umetolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyo chini ya rais wake Leodegar Tenga kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari leo mchana.
Taarifa imesema kwa mujibu wa kalenda ya mashindano (roadmap), mashindano ya Copa Coca-Cola ngazi ya wilaya yanatakiwa kufanyika na kukamilika ndani ya mwezi Mei mwaka huu ili baadaye kuendelea na hatua inayofuata.
TFF imewataka wanachama wake (vyama vya vya mikoa) wajipanga kuendelea na mashindano wakati suala la vifaa na fedha likiendelea kufuatiliwa kwa mdhamini wa mashindano.
“Vifaa na fedha zitapatikana wakati wowote baada ya taratibu husika kukamilika. Vifaa kwa ajili ya mashindano hayo vimeagizwa kutoka nje ya Tanzania. Ni matumaini yetu kuwa tutakuwa na mashindano mazuri mwaka huu kulinganisha na msimu uliopita,”imesema taarifa hiyo.
Kampuni ya Coca Cola ilianza kudhamini mashindano hayo mwaka 2007, na tangu mwaka huo yamekuwa yakifanyika kila mwaka.