![]() |
Yanga wakijifua Uwanja wa Gombani Pemba leo asubuhi |
KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amesema kwamba kambi ya Pemba iko shwari na wachezaji wako tayari kuwapa raha mashabiki wa timu yao Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Simba SC.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kisiwani hapa, Niyonzima ambaye amezushiwa kutokweka kwenye kambi ya Yanga, kwanza alikanusha uvumi huo na pili akasema ‘Lazima mnyama afe Jumamosi’.
Niyonzima ambaye ni Nahodha wa Rwanda, Amavubi, amesema kwamba ujio wao kisiwani Pemba, umewapa faraja kubwa sana katika maandalizi yao ya mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba.
![]() |
Niyonzima kulia na kocha Ernie Brandts kushoto Gombani leo |
“Mashabiki wa timu ya Yanga wakae tayari kusherehekea ubingwa wao Jangwani kwa furaha kubwa baada ya kuwafunga mahasimu wetu wa jadi Simba,”alisema.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Freddy Felix Minziro, alisema amasikitishwa sana na baadhi ya vyombo vya habari leo nchini kuzusha Niyonzima ametoweka Pemba.
“Nashangaa kuona vyombo vya habari vinatoa taarifa ambazo siyo za ukweli, Haruna huyu hapa tunaye Pemba, wala hajaondoka kwenda popote pale,”alisema.
Beki huyo wa zamani wa pembeni wa Yanga aliyeanzia kucheza wingi, amewataka wana Yanga kuondokana na hofu iliyotanda ya kuondoka kwa kiungo wao huyo, jambao ambalo sio la kweli.
Yanga imeendelea na mazoezi yake leo kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba, baada ya jana kufanya mazoezi maeneo ya Vitongoji na kuwafanya mashabiki waliojitokeza Gombani jana kuikosa timu hiyo.
![]() |
Kocha wa makipa, Razack Ssiwa akiwa na rubani wa ndege iliyowapeleka Pemba Ijumaa |
Yanga ilianza mazoezi leo asubuhi majira ya saa 3:15 hadi saa 5:30 na mashabiki wengi walijitokeza kuangalia mazoezi hayo.
Mmoja wa mashabiki wa hao, Mohammed Saulu Ali, kutoka kisiwani kwa binti Abeid, alisema kwamba, ujio wa timu hiyo umewapa faraja kubwa sana, kwani mara nyingi wamekuwa wakiiona Yanga katika Televisheni tu.
Yanga ilifika hapa Ijumaa jioni kwa ndege maalum ya kikodi na kuweka kambi katika hoteli ya Samail, mkataba la na beki ya PBZ kujiandaa na mchezo huo, ambao wamepania kulipa kisasi cha 5-0 walizofungwa msimu uliopita.
Na watani wao wa jadi, Simba SC nao wamejificha maeneo ya Nungwi kisiwani Unguja tangu jana jioni.