• HABARI MPYA

    Tuesday, August 05, 2014

    SIMBA SC YAIPIGA BAO YANGA SAINI YA BEKI LA COASTAL

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeingia Mkataba wa miaka mitatu na beki Abdi Banda kutoka Coastal Union ya Tanga, ambaye msimu uliopita alikaribia kuhamia kwa mahasimu, Yanga SC.
    Banda amesaini leo Mkataba huo mjini Dar es Salaam na mara moja anatarajiwa kujiunga na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, chini ya kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic.
    Uongozi wa Coastal Union msimu uliopita uliilalamikia klabu ya Yanga SC kumrubuni mchezaji wao huyo ajiunge nao katika dirisha dogo Desemba mwaka jana.
    Abdi Banda akisaini Simba SC leo

    Hata hivyo, Yanga SC haikufanikiwa kumpata mchezaji huyo aliyekuwa ndani ya Mkataba na Wagosi hao wa Kaya- na haijulikani kama waliendelea na mpango huo au la, lakini kijana ametua Simba SC.
    Banda anayemudu kucheza nafasi zote za ulinzi, ingawa beki ya kushoto ndipo alipopatia umaarufu hadi kuitwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20- ni miongoni mwa vijana wadogo nchini wenye vipaji wanaotarajiwa kuwa nyota wa soka ya Tanzania baadaye. 
    Tayari Simba SC imewasaini makipa Peter Manyika, Hussein Sharrif ‘Cassilas’, mabeki Jerome Mvengere, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Shaaban Kisiga na washambuliaji Ibrahim Ajibu na Elias Maguri.
    Wekundu wa Msimbazi pia wapo kwenye harakati za mwishoni za kumsaini kiungo Mrundi, Pierre Kwizera ambaye tayari nchini na mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAIPIGA BAO YANGA SAINI YA BEKI LA COASTAL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top