• HABARI MPYA

    Tuesday, November 11, 2014

    DENI LA NDUMBARO LAIHENYESHA TFF, MILIONI 45.8 ZAMTOA KIJASHO CHEMBAMBA MALINZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAKILI Damas Ndumbaro analidai Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sh, Milioni 45.8, ambazo shirikisho hilo linampiga chenga kumlipa.
    Habari za kiuchunguzi ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka TFF, zinasema kwamba deni hilo linatokana na Ndumbaro kuandaa mechi kati timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Afrika Kusini, Bafana Bafana.
    Katika mchezo huo, uliofanyika Jumamosi ya Mei 14, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Bafana ilishinda 1-0, bao pekee la Doctor Siyabonga Sangweni dakika ya 44.
    Ndumbaro alisimama kama muandaaji wa mechi ambaye pamoja na kuchukua asilimia 25 ya mapato yote ya mechi kutokana na mauzo ya tiketi, pia aliingia Mkataba na TFF kulipwa mamilioni.
    Wakili Damas Ndumbaro anaidai TFF Milioni 48.5 ambazo anapigwa chenga kulipwa

    TFF, wakati huo chini ya Rais wake, Leodegar Chilla Tenga ilishindwa kumlipa Ndumbaro fedha hizo na ameendelea kudai hadi baada ya uongozi mpya kuingia madarakani chini ya Rais, Jamal Emil Malinzi.
    Alipoulizwa jana kuhusu deni hilo la Ndumbaro, Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa alikiri kweli lipo, lakini akasema hawezi kulizungumzia kwa sababu yuko kwenye mkutano.
    Kwa upande wake, Wakili Ndumbaro alipoulizwa kuhusu deni hilo, alisema; “Mambo yote yanayohusiana na TFF siwezi kuyaongea, nilikwishamaliza kuongea, chochote kinachohusiana na TFF siwezi kuongea, ikitokea ishu nitaitisha Mkutano na Waandishi wa Habari, nitazungumza kwa pamoja,” alisema jana.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi anakwenda kulipa deni la Ndumbaro

    Ndumbaro ameongeza kwamba hawezi kukumbuka anadai kiasi gani na wapi, kwa sababu hadi sasa anadai zaidi ya Sh. Milioni 600 kwa watu mbalimbali.
    “Siwezi kukumbuka nadai kiasi gani kwa nani kwa sasa, kwa sababu ninawadai watu wengi, wengi sana. Siwezi kuwaweka wadeni wangu wote hadharani, kwa sababu nadai zaidi ya Sh. Milioni 600,”amesema.
    Siri ya deni hili, inafichuka wakati tayari Ndumbaro amefungiwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa miaka saba kujishughulisha masuala ya soka, baada ya kukutwa na hatia ya kuandaa uasi dhidi ya shirikisho hilo. Lakini tayari Ndumbaro amekata Rufaa TFF juu ya adhabu hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DENI LA NDUMBARO LAIHENYESHA TFF, MILIONI 45.8 ZAMTOA KIJASHO CHEMBAMBA MALINZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top