• HABARI MPYA

    Wednesday, November 12, 2014

    MOROCCO NI EBOLA, HAYA CECAFA WATUAMBIE NINI KIMETOKEA ETHIOPIA?

    KINACHOSUBIRIWA ni tamko rasmi la Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kwamba michuano ya Challenge haitafanyika mwaka huu.
    Lakini tayari dalili zote zimetosha kutoa majibu kwamba, CECAFA Challenge haitafanyika mwaka huu, kufuatia waliokuwa wenyeji Ethiopia kujitoa.
    CECAFA iliiomba Sudan kuwa mwenyeji wa Kombe la Challenge mwaka huu, michuano iliyopangwa kuanza Novemba, yaani mwezi huu lakini nayo imekataa.
    Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alikaririwa akisema kwamba, Shirikisho la Soka la Sudan lingetoa majibu kabla ya mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini hadi jana hakukuwa na majibu yoyote. Sudan wamekuwa wepesi wa kukubali uenyeji wa michuano ya CECAFA, kwa sababu wanajiweza kifedha.

    Ni Sudan waliokuwa wenyeji wa michuano ya kwanza ya CECAFA, Nile Basin katikati ya mwaka huu.
    CECAFA ilileta michuano hiyo mipya inayoshirikisha mabingwa wa Kombe la FA au washindi wa pili wa Ligi Kuu za nchi wanachama wake, ili kuongeza changamoto.
    Michuano mingine ya klabu kwa CECAFA ni ile mikongwe ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame, ambayo mwaka huu ilifanyika Kigali, Rwanda na El Merreikh ikabeba taji.
    CECAFA ilikuwa ina michuano mingi hadi ya vijana ya mataifa, ambayo yote imeshindwa kufanyika kutokana na nchi wanachama wake kutokuwa tayari kuubeba mzigo huo.
    Challenge iliyofanyika Kenya mwaka jana na wenyeji kuwa mabingwa ilikuwa kichekesho- ilihamishwa kutoka jimbo moja hadi lingine kwa sababu ya kuwapelekea mashindano Magavana waliochangia fedha.
    CECAFA na wenyeji FKF walishindwa kuzilipia malazi baadhi ya timu hadi zikazuiwa kuondoka hata zilipotolewa kwenye mashindano.
    Kwa ujumla, miaka kadhaa sasa michuano ya CECAFA imekua ikifanyika kwa dhiki na dhalili sababu ya kutokuwa na bajeti ya kutosha ya kuiendeshea.
    Sababu kubwa ya michuano hiyo ya CECAFA kufanyika ‘kimkandamkanda’ ni uongozi wa Baraza hilo kukosa mpango mkakati na ubunifu- zaidi viongozi wake kutowajibika ipasavyo.
    Nchi zote wanachama wa CECAFA zipo tayari kushiriki michuano hiyo, lakini si kuwa wenyeji kutokana na ukweli kwamba haina mvuto tena.
    Nchi zimekuwa zikiomba uenyeji wa michuano hiyo pale zinapohitaji kwa sababu zao binafsi, kama Kenya mwaka jana walitaka kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wao.
    Rwanda tayari wameomba kuwa wenyeji wa michuano ya mwakani, kwa sababu wanataka kutumia fursa hiyo kama sehemu ya kujipima kabla ya michuano ya CHAN.
    Na bado wakati Challenge na Kagame pekee inakuwa mzigo kwa CECAFA, Baraza hilo limeleta michuanio mingine tena ya Nile Basin.
    Na wanaleta michuano hiyo wakiwa hawana mkakati wowote, zaidi ya kuzitegemea nchi ndiyo ziubebe mzigo huo.
    CECAFA inashindwa kujua kwamba wanachama wake sasa wanafunguka na kujitambua zaidi kiasi cha kuwa na matamanio zaidi, ikiwemo kushiriki fainali za mashindano makubwa kama CHAN, AFCON na Kombe la Dunia.
    Wangejua hivyo, basi wangeboresha zaidi mashindano hayo ya Challenge yakawa na mvuto ili kutengeneza ushawishi wa nchi wanachama wake kuwa tayari kuyagombea kuandaa.
    Maofisa wa CECAFA wanapokwenda kusimamia mashindano, watataka malazi, usafiri na posho zao viwe tayari, lakini wana mchango gani katika kufanikisha mashindano hayo? Haijulikani.
    Tulitarajia mwisho wa Challenge iliyopita Desemba mwaka jana, uwe mwanzo wa Challenge ya mwaka huu, lakini wapi- katika wiki ya mwisho kuelekea mashindano, wenyeji wanajitoa. Lazima kuna mushkeli hapo.
    Morocco wamepokonywa uenyeji wa AFCON ya mwakani kwa sababu ya msimamo wao kutaka mashindano yasogezwe mbele kwa miezi sita kutokana na hofu ya ugonjwa wa Ebola.
    Hiyo imeeleweka, lakini Ethiopia wana sababu  gani ya kujitoa dakika za mwishoni kuandaa michuano hiyo? Wakati umefika viongozi wa CECAFA wafunguke zaidi kifikra na mipango kama kweli wanataka kuivusha soka ya ukanda huu katika hatua nyingine, vinginevyo, tutaendeela kuwa mwisho wa milele. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MOROCCO NI EBOLA, HAYA CECAFA WATUAMBIE NINI KIMETOKEA ETHIOPIA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top