• HABARI MPYA

    Thursday, May 17, 2012

    MAESTRO WA SIMBA MAFISANGO AFARIKI DUNIA




    KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango wa Simba, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Tazara, Dar es Salaam.
    Mafisango amefariki kwa ajali ya gari akiwa anarejea nyumbani kwake, kutoka disko na kwa sasa mwili wake upo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
    Meneja wa Simba SC, Nicodemus Menard Nyagawa amethibitisha kifo cha mchezaji huyo na amesema hilo ni pigo kubwa  kwa klabu hiyo.
    Nyagawa alisema Mafisango aliyekuwa anaendesha mwenyewe gari lake, alikuwa anajribu kumkwepa dereva wa pikipiki na kwa  bahati mbaya akaingia mtaroni na kuumia kabla ya kufariki dunia. 
    Mafisango aliyekuja nchini mwaka juzi na kujiunga na Azam kabla ya kuhamia Simba mwaka jana, alizaliwa Machi 7, mwaka 1987 mjini Kinshasa, DRC alikoanzia soka kabla ya kuhamia Rwanda, ambako baadaye alichukua uraia wa nchi hiyo.
    Kabla ya kuja Tanzania alichezea APR ya Rwanda. Mechi ya mwisho Mafisango kuichezea Simba ilikuwa dhidi ya Al Ahly Shandy nchini Sudan Jumapili katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penalti 9-8, kufuatia sare ya jumla ya 3-3.
    Hadi anafariki dunia, Mafisango alikuwa ni tegemeo na jana tu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nange Kaburu alisema kiungo huyo yupo kwenye mpango wa kocha wa kikosi cha msimu ujao. Poleni wana Simba wote, pole kwa ndugu, jamaa na familia ya Mafisango. Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe milele. Amin. Mungu iweke pema peponi Roho ya Marehemu. TAARIFA ZAIDI ZINAKUJA:

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAESTRO WA SIMBA MAFISANGO AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top