![]() |
Wachezaji walioipa Azam Medali ya Fedha Ligi Kuu msimu uliopita |
Na Prince Akbar
KLABU ya Azam FC inaendelea vema na maandalizi yake ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame na leo asubuhi walifanya mazoezi
katika ufukwe wa Coco Beach, Dar es Salaam.
Azam ilianza mazoezi ya viungo na kusaka pumzi na stamina wiki
mbili zilizopita, Beach na Gym na wiki wanatarajiwa kuanza kuuchezea mpira.
Tayari Azam, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara wamekwishamalisha usajili wa wachezaji wao hata kabla ya kwenda
likizo.
Programu ya maandalizi ya Kombe la Kagame, inayoendelea hivi
sasa itamalizika siku moja kabla ya kuanza mashindano hayo, Juni 28 na
yatakapomalizika, wachezaji watapewa mapumziko ya siku chache kabla ya kuanza
maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
Maandalizi kwa ajili ya VPL yatahusisha pia ziara ya nje ya
nchi ya kujiandaa na msimu mpya, ingawa amesema nchi hiyo itatajwa baadaye.
Wachezaji wapya kikosini Azam msimu huu ni kiungo Mkenya
George ‘Blackberry’ Odhiambo na kipa Deogratius Munishi kutoka Mtibwa Sugar,
wakati Aishi Salum, Jackson Wandwi, Dizana, Ibrahim Rajab Jeba na Joseph
Kimwaga, wamepandishwa kutoka akademi ya Azam.
Kikosi kamili cha Azam FC kinaundwa; na makipa, Mwadini
Ally, Deo Munishi ‘Dida’ Aishi Salum na Jackson Wandwi, mabeki wa Ibrahim Shikanda,
Erasto Nyoni, Waziri Salum, Samir Haji Nuhu, Luckson Kakolaki, Said Mourad,
Joseph Owino na Aggrey Morris.
Viongo ni Kipre Bolou, Abdulhalim Humud, Himid Mao, Salum
Abubakar, Abdi Kassim Sadalla, Ramadhani Suleiman Chombo, Abdulghani Ghullam,
Ibrahim Rajab Jeba, Jabir Aziz Stima, Ibrahim Joel Mwaipopo, Kipre Tchetche,
Mrisho Ngassa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha na George Odhiambo ‘Blackberry’ wakati
washambuliaji ni Gaudence Mwaikimba, John Bocco ‘Adebayor’.
Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kucheza Kombe la Kagame, baada
ya kushika nafasi ya pili katika msimu uliopita wa Ligi Kuu. Katika Kombe la
Kagame mwaka huu, wenyeji Bara wataingiza timu tatu, Yanga ambao ni mabingwa
watetezi, wakati Simba na Azam wanaingia kwa nafasi za uwakilishi.
0 comments:
Post a Comment