![]() |
Uwanja wa sasa wa Azam |
KLABU ya Azam FC, imeanza ujenzi wa Uwanja mpya mkubwa na wa
kisasa wenye hadhi sawa na Uwanja mpya wa Taifa wa Dar es Salaam, ambao ndio
utakuwa ukitumika kwa mechi mbalimbali za timu hiyo, wakati Uwanja wa sasa
utakuwa kwa ajili ya mazoezi tu.
Habari za ndani kutoka Azam (siyo kwa Patrick Kahamele),
ambazo BIN ZUBEIRY imezipata zimesema kwamba tayari hatua za awali za
ujenzi zimeanza katika eneo lile lile la Chamazi.
“Tunajenga Uwanja mwingine mkubwa, huo utakuwa kama Uwanja
wa Taifa. Utakuwa unatumika kwa mechi zetu zote za kitaifa na kimataifa, huu Uwanja
wa sasa utakuwa kwa ajili ya mazoezi tu na mechi za timu za vijana,”kilisema
chanzo chetu kutoka Azam.
Azam FC wanaelekea kupiga hatua nyingine kubwa na kuzidi
kuzipiga bao, timu kongwe nchini Simba na Yanga- kwani hadi sasa tayari hiyo ndio
klabu pekee nchini yenye Uwanja wake wenye kukidhi vigezo.
Simba iliyoanzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita, bado haina Uwanja
hata wa wachezaji wake japo kupigia danadana, wakati wapinzani wao wa jadi, timu
kongwe zaidi nchini kwa sasa, Yanga ina Uwanja wa Kaunda, ambao umetelekezwa na
upo katika hali isiyotazamika.
Ingawa historia inasema Yanga ilizaliwa mwaka 1935 na Simba
mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa
utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938
ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa
ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs,
vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani
kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina
Jangwani.
Ndani ya kipindi kifupi tu, timu hiyo iliteka hisia za
wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo. Miongoni mwa
waliovutika na uanachama wa klabu hiyo ni Tarbu Mangara (sasa marehemu) na
ilipofika mwaka 1926, walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi kuna
shule ya sekondari ya Tambaza.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha
timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na
mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
Baada ya mkutano huo, timu hiyo ilibadilishwa jina na kuwa
Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi
hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na
Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana Jangwani hao.
Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu
hiyo walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo
zaidi. Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye
ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu
yao na kuiita Taliana.
Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza
ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka
ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye
ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya
vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum,
lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati
baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu
hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo
mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema
Yanga.
Azam FC, ilianzishwa mwaka 2004 tu na kikundi cha
wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao
yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said
Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya
kazi.
Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka
2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia
jina la Mzizima FC.
Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa,
aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na
kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam
Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika. Wazo lake
lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa
Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa
jina tena na kuwa Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi
mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, na msimu uliopita pamoja na kutwaa
Kombe la Mapinduzi mbele ya vigogo wa soka nchini Simba na Yanga, pia ilikaribia
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu- baada ya kuzidiwa na Simba waliobuka mabingwa, huku
wao wakishika nafasi ya pili mbele ya waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga.
Kwa mara ya kwanza, Azam mwakani itapeperusha bendera ya Tanzania
kwenye michuano ya Afrika, ikicheza Kombe la Shirikisho.
0 comments:
Post a Comment