![]() |
Mbwana Ally Samatta wa TP Mazembe, akimshughulisha Kolo Habib Toure wa Manchester City |
DIDIER Drogba, akiwa na urefu wa futi sita na mng�ao wa pesa anajitokeza katika korido za vyumba vya kubadilishia nguo katika Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny. Nyuma yake kuna rundo la wachezaji wenzake mastaa.
Nabaki nimeduwaa.Mtu ambaye wiki chache zilizopita alikuwa mbele ya televisheni yangu akiifanyia maajabu Chelsea.
Anatazama jezi yangu iliyoandikwa jina �Tanzania� kifuani. Anatabasamu ananipa mkono ananisalimia kisha ananiambia �karibu Ivory Coast�.Sipati muda wa kuongea naye taratibu anaanza kuondoka nyuma yake kuna Cheikh Tiote, Kader Keita, Yaya Toure, Kolo Toure, Emmanuel Eboue na wengineo.
Wakati anakaribia kuchomoza katika sehemu ya uwanjani, anasita, anageuka nyuma, anatabasamu.Anajisikia aibu kwa sababu anajua uwanja mzima unamsubiri yeye.
Eboue anamsukuma kwa utani.
Ghafla anajitokeza uwanjani huku wenzake wakimfuat anyuma. Uwanja mzima unapagawa, mashabiki wanapiga kelele za kuchanganyikiwa kwa kumuona kwake. Ni kama vile limefungwa bao la fainali katika uwanja wa nyumbani. Na mimi nachanganyikiwa.
Anageuka upande wa kulia anapunga mkono hewani, anageuka upande wa kushoto anapunga mkono hewani.
Mashabiki wanapagawa.Uwanja mzima unachanganyikiwa kumuona mfalme huyu.
Wachezaji wenzake hawana habari.Kila mmoja yuko na mwenzake anapiga stori.
Lakini Drogba anageuzwa kuwa tukio maalumu katika uwanja wa Felix Houphouet-Boigny.
Hatimaye anatembea taratibu kwa maringo kwenda upande wa kulia kuwasalimia mashabiki.
Upande ule wa kulia watu wanachanganyikiwa, wanakanyagana kwa ajili ya kusogea mbele kumuona kwa karibu. Kundi kubwa la askaril inafanya juhudi kubwa kumzunguka. Na mlinzi wake binafsi anasimama nyuma yake.
Kisha anageuza, anavuka uwanja na kwenda upande wa kushoto ambako kama ilivyo kwa Uwanja wa Taifa, kuna televisheni kubwa. Kule nako watu wanapagawa, akili zinawaruka, wanakanyagana kusogea mbele kumuona kwa karibu. Mwishowe anarudi zake kuungana na wenzake.
Si Toure wala Tiote wanaofanya hivyo.Ni yeye peke yake. Ana kitu cha ziada katika ubongo wa watu wa hapa.
Anatimka zake kwenda vyumbani na wenzake, lakini ghafla anakutana na waamuzi wa mechi ambaoni Waraabu.
Anamsalimia mmoja mmoja kwa heshima kubwa na watu wanashangilia. Unajiuliza, wanashangilia nini hasa? Lakini katika akili yangu nafahamu kuwa anacheza mchezo wa akili kwa kuwavuta waamuzi upande wake ili wampe heshima maalumu uwanjani.
Dakika kadhaa baadaye, Mfalme Drogba anafanya jambo la kipuuzi kidogo.Yeye ni nahodha, na amesimama mbele karibu na waamuzi kando ya nahodha wetu, JumaKaseja.
Lakini wakati mwamuzi akiamrisha timu zianze kuelekea uwanjani, Drogba anainama chini na kuanza kufunga taratibu kamba zake za viatu pamoja na plasta ya nje ya soksi.Inachukua dakika tano.
Anafanya hivi taratibu na wachezaji wa timu zote mbili ambao wako tayari kutoka kuelekea uwanjani wanalazimika kumsubiri.
Kaseja kasimama kando na anashangaa jinsi nahodha mwenzake anavyojifanyia mambo yake kwa namna anavyotaka. Timu zinachelewa kutoka uwanjani.
Baada ya kuingia uwanjani, ndani ya dakika tano mpira unaanza.Uwanja mzima unamtazama mtu huyu anayekaribia kulipwa pauni 250,000 kwa wiki pale China.
Haonekani kuwa makini sana kama tunavyomuona darajani. Anacheza huku anatembea.
Muda mchache baadaye anapokea mpira na Aggrey Morris anamkwatua kidogo tu kwa nyuma.
Drogba anajirusha kama amechotwa na katapila. Morris anapewa kadi ya njano.Hapo hapo nakumbuka jinsi Drogba alivyo wasalimia kwa bashasha waamuzi wakati wanaenda kupasha misuli moto.
Muda mchache baadaye inakuwa zamu ya Shaaban Nditi.Anamuingia kwa nguvu nyuma na Drogba anajirusha kama Bruce Lee.
Bahati kwa Nditi hapewi kadi ya njano lakini faulo inapigwa kuelekea lango la Stars. Anapiga mwenyewe,anapaisha, anacheka.Uwanja unapiga makofi.
Kwa dakika zote tisini, Drogba haonekani kuwa makini uwanjani. Na kila akijaribu kuwa makini Kelvin Yondani na Morris wanamdhibiti vilivyo.
Hapumui.Kitu kizuri ni kwamba hana dharau. Anaongea vizuri na akina Yondani uwanjani wakati mech iinaendelea.
Baadaye anafunga kwa kichwa kwa staili ileile ya usiku wa Allianz Arena. Uwanja mzima unazizima.Bao la Kalou lilikuwa zuri kuliko la Drogba, lakini hili linashangiliwa sana kwa sababu limefungwa na Mfalme.
Mpira unakwisha, wachezaji wa Stars wanahaha kupiga naye picha na wala haonyeshi maringo.
Hata mimi najisogeza na kupiga naye picha.Natafuta nafasi ya kuonge naye naikosa, kila mtu anamzunguka yeye, wapiga picha wote wanamzunguka yeye.
Ghafla akachomoka kwenda katika mashabiki wa jukwaa la kushoto ambao wakati ule aliwafanya watu wa mwisho katika salamu zake. Kabla hajafika, kijana mmoja anapenya na kuingia uwanjani kwa kasi akielekea kumkumbatia Drogba.
Maaskari wanamzunguka na kuanza kumchapa.
Drogba anawahi katika tukio na kuamrisha askari wasimpige. Anamkumbatia na askari wanatulia kama vile wamepewa amri ya kijeshi.
Anakimbia na kijana huyo kwenda kumpandisha ngazi za jukwaani na kifupi ni kwamba anaokoa maisha yake kutoka kwa askari wenye hasira ambao majuzi tu walikuwa wakishiriki vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Baada ya hapo uwanja mzima unamshangilia.Anateka kila kitu uwanjani.Hakuna anayejishughulisha naTiote, Gervinho wala Toure ambaye wiki chache tu zilizopita kawapa ubingwa Manchester City.
Katika mkutano na waandishi wa habari simuoni Drogba. Nilitazamia angekuwepo, lakini anakuja Solomoni Kalou na kocha wake,Sabri Lamouchi.
Wanaongea lakini na mimi akili yangu imetekwa na Drogba.
Bahati nzuri ukumbi wa waandishi wa habari uko upande ule ule ambao kuna vyumba vya wachezaji wa Ivory Coast.
Namsikiliza Kalou haraka haraka kisha kocha wake. Wote wanaisifia Tanzania, wote wanamsifia Mbwana Samatta.Napata kitu cha kuandika kisha naondoka kumnyemelea Drogba.
Ghafla wachezaji wa Ivory Coast wanaanza kujitokeza kwenda nje kupanda basi. Wanapita wote akina Eboue najifanya siwaoni, ghafla anatokeza mfalme.
Hii ndio fursa pekee ya kupata neno kutoka kwake.Namuwahi fasta kabla waandishi wengine hawajanusa.
Namuuliza ameionaje Stars, anasema imecheza bonge la mechi na hakutegemea hivyo. Namuuliza nan iamekuvutia,anajibu �yule aliyevaa jezi namba 10�.
Anamwagia sifa Samatta na mwishowe anatania kwa kusema �anawezakwenda Stamford Bridge kuvaa jezi yangu, mimi naondoka, mwambie aende�. Moyo wangu unafarijika.Nataka kumuuliza kitu, kumbe kundi la waandishi limeshatuzunguka.Mmoja ananiwahi na kumuuliza Kifaransa, mwingine tena anauliza hapo hapo.
Tulikuwa wawili, lakini ghafla tukajikuta tuko 40.Najichomoa kundini.
Walinzi wanamzuia asijibuma swali.Anaondolewa kwa nguvu. Nageuka kumtazama anavyotokomea, natabasamu.Hapo hapo nakumbuka ile penalti yake ya mwisho pale Allianz Arena. Mfalme anatoweka machoni kwangu!
SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI:
0 comments:
Post a Comment