KIUNGO Ibrahim Rajab Juma Jeba amesisitiza kwa sasa ndoto yake ni kujiunga na Simba licha ya kuwekewa zengwe na timu yake ya Azam. "Ndoto yangu katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ni kuvaa jezi za rangi nyeupe na nyekundu," anasema Jeba. Ndoto ya Jeba huenda ikayeyuka kwani Azam imewasilisha malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga usajili wake. Jeba, ambaye amejazia kwa mazoezi anasifika kwa kujituma na kuwa msumbufu uwanjani. Ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao. Amesaini mkataba wa miaka miwili. Sakata hilo la kuzuiwa na Azam linamnyima raha mchezaji huyo. Kutokana na mkasa huo, Mwanaspoti ilizungumza na Jeba kwa kirefu juu ya mkasa huo na yeye anaeleza pamoja na malengo yake. Mvutano wake na Azam Jeba anaizungumzia Azam kuwa ni klabu bora kwake, lakini hakuwa na bahati nayo kwa sababu licha ya kucheza kikosi cha timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 kwa mafanikio katika michuano mbalimbali, lakini ilishindwa kumwamini na kumjumuisha katika timu ya wakubwa. "Azam ni bora kwangu kutoka waliponitoa hadi hapa nilipo ni juhudi zao,"anaeleza Jeba anayeishabikia klabu ya Chelsea ya England na anavutiwa na soka ya Mbrazili Ricardo Kaka wa Real Madrid. Akizungumzia mkasa wake wa usajili, Jeba anasimulia kuwa walikubaliana na Azam wamwache na walitekeleza hilo kwani kwa muda mrefu walikuwa hawamlipi mshahara. "Ninachowaambia Azam nawaomba waniache kama tulivyokubaliana, wasiniwekee vikwazo kwa sababu mimi ni kijana natafuta maisha, waniache nijaribu bahati lakini si kuniwekea pingamizi,"anaeleza kwa masikitiko. Meneja wa klabu hiyo, Patrick Kahemele anasema, Jeba ni mchezaji wao na kudai kuwa Simba wamempora mchezaji wao. Kahemele alifananisha kitendo kile na kitendo cha Chelsea kumnyakua Gael Kukuta wa Lens ya Ufaransa. "Jeba ni mchezaji wa timu ya yosso ya Azam hata bila mkataba anafungwa, lakini pia ana mkataba na Azam uliosainiwa Novemba 2011 na ikamtoa mkopo kwenda Villa Squad. Huko hakwenda kwani alikuwa anaumwa mguu. "Kitendo cha Simba kufanya naye mazungumzo, kumhamisha kinyemela na kufanya nao mazoezi ni uvunjifu wa kanuni za soka kama si kuleta vurugu tulizoanza kuzisahau." Sababu ya kujiunga Simba "Nimejiunga Simba kutokana na mpango wao wa kuendeleza vijana kwani idadi ya wengi walioko hapo wamefanikiwa kutokana na kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza,"anasema na kutolea mifano kwa Shomari Kapombe, Edward Christopher, Abdallah Seseme, Ramadhan Singano Messi na Jonas Mkude. "Lakini pia, Simba ninaipenda tangu nilipokuwa mdogo, nilitamani siku moja niichezee na sasa nimekamilisha ndoto zangu. "Kingine ni maslahi kwa sababu mpira ndiyo ajira yangu na pia nilitaka kubadilisha mazingira kuona kama naweza kutimiza ndoto zangu,"anaeleza Jeba na kudokeza, mmoja wa viongozi wa Simba alichangia huduma ya matibabu, alipokuwa amevunjika mguu na kuwekwa bandeji ngumu (P.O.P). Aliumia katika mechi ya fainali ya Kombe la Uhai mwaka jana kati ya Azam na Simba. Anaongeza na kusema kutokana na mapenzi pamoja na kujituma, anaamini atafanikiwa kwani atajibidiisha na kufuata maelekezo ya kocha wa Simba, Milovan Cirkovic kwa ufasaha na kuahidi hawatajutia usajili wake. Jeba anazungumzia pia ushindani wa namba, kwani katika kikosi cha Simba, anafahamu atakuwa na kibarua cha kugombea namba na wakali kama Haruna Moshi Boban, Mwinyi Kazimoto na Mzambia Felix Sunzu. "Wale ni wakubwa wangu na wananizidi ujuzi lakini nafahamu utafika wakati wangu nami nitapata nafasi." Chanzo cha kutungiwa jina Jeba Jeba anasema jina hilo lilitungwa na watu wa karibu yake na lilikuwa zaidi kutokana na kucheza kwake soka. "Nilipewa jina hili na watu wa karibu yangu na wao walikuwa na maana kuwa, pamoja na umri wangu mdogo niliokuwa nao, nilionekana kama na umri mkubwa ndio wakaniita jina la Jeba. "Licha ya muonekano wangu, lakini niliweza kupambana na walio wakubwa zaidi yangu, ndipo likaendelea kukua, likazoeleka mpaka sasa,"anaeleza Jeba na kuongeza analifurahia jina hilo. Alivyopenya katika soka Jeba anasema kipaji chake kilianza kuonekana tangu alipokuwa mdogo na aliyechangia sehemu kubwa ya mafanikio yake ni baba yake mzazi, Mzee Ibrahim Rajab. "Kipaji changu kilianza kujionyesha tangu nikiwa mdogo nilipoanza Shule ya Msingi ya Mwanakwerekwe huko Zanzibar na nilishiriki mashindano mbalimbali. "Soka la ushindani nilianza katika timu yangu ya mtaa, Simba Kids ambayo pia niliihama 2005 na kujiunga na Lebanon. "Nilipokuwa Lebanon mwaka 2007, klabu ya Ras El Khalima ilinichukua kwa ajili ya michuano ya Ligi Daraja la Kwanza la Zanzibar ambayo pia sikukaa nayo sana nikajiunga na Ochu Boys yenyewe ilikuwa Ligi Daraja la Pili,"anasema Jena na kuweka wazi sababu zilizomsababishia kuhamahama kwa ajili ya kutafuta njia ya kutoka na maslahi. Hali hiyo ndiyo ilimsaidia pia, kwani mwaka 2010 alivyokuja na timu ya Mkoa wa Mjini Magharibi ya Zanzibar katika michuano ya Copa Coca Cola, Azam ilimwona na kumjumuisha katika kikosi chao cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 kabla ya kujiunga na Simba, msimu huu. Alizichezea pia timu za taifa za vijana Tanzania, chini ya miaka 17, chini ya miaka 20 na chini ya miaka 23, lakini pia alikuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' kilipokuwa kikijiandaa na mashindano ya Kombe la Chalenji mwaka jana na kwenda nayo kambini Misri. | ||
SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI:
0 comments:
Post a Comment