![]() |
Wachezaji wa Simba waliokuwa mazoezini juzi |
HADI sasa kwenye Uwanja wa TCC Chango’ombe, Dar es Salaam
ambako mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba SC wanaendelea na mazoezi
kujiandaa na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, hakuna mchezaji aliyeongozeka
kutoka idadi ya juzi, wachezaji 13.
Kwa mujibu wa Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ambaye
muda huu tayari yuko maezoini TCC, wachezaji waliokuwa na timu ya taifa nchini
Msumbiji na wengine wapya, akiwemo Danny Mrwanda bado hawajafika.
Kwa maana hiyo, Kiggi Makassy aliyesajiliwa kutoka Yanga
ndiye anaendelea kuwa mchezaji ‘lulu’ kwenye mazoezi hayo.
Juzi BIN ZUBEIRY ilitembelea mazoezi ya
Simba TCC na kukuta wachezaji 13 wakijifua chini ya Kocha Msaidizi, Mganda Hamatre
Richard, akiwemo Kiggi Makassy ingawa mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Dong
Tam Long An ya Vietnam, Danny Davis Mrwanda hakutokea.
Mashabiki wengi wa Simba walifika mapema Uwanja wa TCC
Chang’ombe, Dar es Salaam kuwashuhudia wachezaji wao, kiu zaidi ikiwa kumuona
mpachika mabao wao wa zamani, aliyerejea kikosini Mrwanda, lakini Meneja wa
Simba, Nico Nyagawa akaiambia BIN ZUBEIRY kwamba mchezaji huyo ni
miongoni mwa waliotoa udhuru.
Waliohudhuria ni pamoja na Salim Kinje, Abdalllah Juma,
William Mweta, Hamadi Waziri, Abuu Hashim, Haroun Athumani, Haruna Shamte, Amri
Kiemba, Paul Ngalema, Uhuru Suleiman, Patrick Kanu Mbivayanga na Abdallah
Seseme.
Mazoezi hayo yaliongozwa na Richard kwa sababu Kocha Mkuu,
Mserbia Milovan Cirkovick bado anakula sikukuu kwao.
Simba itaendelea na program ya mazoezi kwa jioni tu wiki hii
na Nyagawa amesema anatarajia idadi ya wachezaji itakuwa ikiongezeka taratibu
wiki hii, wakiwemo wachezaji waliokuwa na timu ya taifa Msumbiji nao pia
wanatarajiwa kuungana na wenzao wakirejea kutoka nchini humo.
Mrwanda ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea
Simba, ambao hauna kipengele cha kumruhusu kuuvunja kabla haujamalizika naye
anatarajiwa kuanza maozezi wakati wowote wiki hii.
Mrwanda, awali ilielezwa anataka kusaini mkataba ambao
wakati wowote akipata timu nje, aondoke, lakini kwa mujibu wa mkataba aliosaini
Simba ni kwamba akipata timu italazimika kumnunua kutoka kwa Wekundu wa
Msimbazi, au isubiri hadi amalize mkataba.
Habari za uhakika, kutoka ndani ya Simba SC ambazo BIN
ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Mrwanda ameridhika na mkataba huo na
ameahidi kufanya vitu baab kubwa Msimbazi.
Kwa upande mwingine, Simba SC imeamua kumtema kiungo Salum
Machaku kwa makubaliano maalum ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba. Simba
ilitaka kumtoa kwa mkopo Machaku, lakini mwenyewe akasema bora aachwe moja kwa
moja.
Tayari Simba imemsajili kiungo wa Yanga, Kiggi Makassy
kuziba nafasi ya Machaku. Machaku sasa ameingia kwenye mazungumzo na Yanga.
0 comments:
Post a Comment