• HABARI MPYA

    Monday, October 01, 2012

    SIMBA SC YATOKA SARE NA MASTAA WA ZENJI

    Simba SC

    Na Princess Asia
    SIMBA SC imetoka sare ya bila kufungana na All Stars ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki jana usiku uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kujiandaa na mechi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC.
    Simba SC inaendelea vizuri na maandalizi yake ya pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, Oktoba 3, mwaka huu, ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislam, Kwerekwe, visiwani Zanzibar na kambi yao ipo Chukwani.
    Morali ya kambi ipo juu na wachezaji wote wako fiti, wakijifua kwa shauku kubwa ili kumvutia kocha Mserbia, Milovan Cirkovick awape nafasi ya kucheza Oktoba 3, kuanzia sa 1:00 usiku.
    Simba ilirejea jana Zanzibar, baada ya juzi kuendeleza wimbi lake la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwa kuichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea Ligi Kuu msimu huu mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba yalitiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho Ngassa, ambaye hilo ni bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ndani ya mechi nne na la pili jumla tangu ajiunge na timu hiyo katika mechi saba alizocheza, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri.
    Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 12 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiizidi Azam FC pointi mbili katika nafasi ya pili, ingawa timu zote zimecheza mechi sawa, nne.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YATOKA SARE NA MASTAA WA ZENJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top