• HABARI MPYA

    Saturday, October 06, 2012

    MECHI YA YANGA NA KAGERA YASOGEZWA MBELE WAGENI WAKIWA WAMEKWISHAFIKA BUKOBA

    Yanga SC

    Na Princess Asia
    KAMATI ya Ligi imesogeza mbele kwa siku moja mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Kagera Sugar na Yanga iliyokuwa ichezwe kesho mjini Bukoba kutokana na Uwanja wa Kaitaba kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba sasa mechi hiyo itachezwa Jumatatu kwenye Uwanja huo huo.
    Wambura alisema kwamba mabadiliko hayo pia yameathiri mechi kati ya Toto Africans na Yanga iliyokuwa ichezwe Oktoba 10 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na sasa itachezwa Oktoba 11 mwaka huu. Yanga tayari wapo Bukoba tangu asubuhi, baada ya kuondoka Dar es Salaam kwa ndege.
    Katika hatua nyingine, Wambura amesema kwa vile msimu huu mdhamini mwenyewe ndiye anayegawa vifaa kwa timu, Kamati ya Ligi imeagiza Vodacom iandikiwe barua na nakala kwa klabu zote ili kujua timu ambazo tayari zimekabidhiwa vifaa hivyo zikiwemo logo na siku ambapo timu husika zilipokea.
    Baada ya majibu ya Vodacom ndipo Kanuni za Ligi Kuu zitakapotumika kutoka adhabu kwa timu ambazo zitabainika kuwa zilipokea vifaa lakini hazikuvitumia. Hatua hiyo inafuatia timu za Yanga na African Lyon kutovaa jezi za wadhamini wa ligi hiyo hadi sasa, kwa sababu mbalimbali.
    Wakati Yanga wanakataa nembo nyekundu kwenye jezi za wadhamini, Lyon wao wana mkataba wa kampuni nyingine ya simu, Zantel.
    Wakati huo huo: Wambura amesema kwamba, Kamati ya Ligi ya TFF iliyokutana jana imepanga Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ianze kutimua vumbi Oktoba 20 mwaka huu.
    Alisema timu zimepangwa katika makundi matatu ya timu nane nane ambapo zitacheza ligi hiyo kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Mshindi wa kila kundi ndiye atakayepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao wakati timu ya mwisho kila kundi itashuka daraja kurudi Ligi ya Mkoa.
    Kundi A lina timu za Burkina Moro ya Morogoro, Kurugenzi Mufindi ya Iringa, Majimaji ya Songea, Mbeya City ya Mbeya, Mlale JKT ya Ruvuma, Mkamba Rangers ya Morogoro, Polisi Iringa na Small Kids ya Rukwa.
    Ndanda FC ya Mtwara, Ashanti United, Green Warriors, Moro United, Polisi, Tessema, Transit Camp na Villa Squad zote za Dar es Salaam ndizo zinazounda kundi B wakati kundi C ni Kanembwa JKT ya Kigoma, Morani ya Manyara, Mwadui ya Shinyanga, Pamba ya Mwanza Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora na Rhino Rangers ya Tabora.
    Ada ya ushiriki wa ligi ni sh. 200,000 zinazotakiwa kulipwa kabla ya Oktoba 13 mwaka huu. Pia Oktoba 13 mwaka huu kutakuwa na kikao kati ya wenyeviti wa klabu zote zinazoshiriki ligi hiyo na Kamati ya Ligi ambapo pia itafanyika draw (ratiba).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECHI YA YANGA NA KAGERA YASOGEZWA MBELE WAGENI WAKIWA WAMEKWISHAFIKA BUKOBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top