• HABARI MPYA

    Tuesday, October 09, 2012

    MILOVAN ASEMA AKUFFO TATIZO KIWANGO NDIO MAANA BENCHI

    Daniel Akuffo mbele ya Mrisho Ngassa

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA Mkuu wa Simba SC, Profesa Milovan Cirkovick amesema kwamba mshambuliaji mpya kutoka Ghana, Daniel Akuffo anatakiwa aongeze juhudi na kupandisha kiwango chake, ili apate nafasi kwenye kikosi cha kwanza, lakini kwa sasa ataendelea kuanzia benchi kwa kuwa anazidiwa uwezo na wachezaji wanaoanza.
    Akizungumza baada ya mechi dhidi ya JKT Oljoro juzi, Mserbia huyo alisema kwamba Akuffo anaanzia benchi kwa sasa kwa sababu kuna wachezaji walio vizuri mno zaidi yake na ndio wanapewa nafasi. “Ajitahidi, atakapokuwa vizuri atapata nafasi ya kuanza, ila kwa sasa anazidiwa na wanaoanza,”alisema Milovan.
    Daniel Akuffo aliyesajiliwa msimu huu kutoka ASEC Mimosa ya Ivory Coast, aliingia kwa kishindo      Simba akifunga katika mechi nne mfululizo, lakini baada ya hapo kasi yake imezimika na amefikisha jumla ya mechi 10, akiwa amefunga mabao matano tu, katika ligi bao moja tu. Katika mabao hayo matano aliyofunga jumla hadi sasa mshambuliaji huyo mrefu, mawili ni ya penalti.
    Simba SC juzi ilizidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 29.
    Kiemba alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na mashambulizi ya upande wa kulia.
    Ilikuwa rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
    Nonga naye alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni kiulaini.
    Bao hilo lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
    Kipindi cha pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao mawili zaidi.
    Dakika ya 83 Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango huyo.
    Awali ya hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti.
    Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi tano.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MILOVAN ASEMA AKUFFO TATIZO KIWANGO NDIO MAANA BENCHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top