• HABARI MPYA

    Saturday, October 06, 2012

    REFA ADUI WA YANGA, SWAHIBA WA SIMBA AENDA NA MAJI LIGI KUU

    Mathew Akrama

    Na Prince Akbar
    KAMA ilivyotarajiwa na wengi, refa Mathew Akrama wa Mwanza aliyechezesha ovyo mechi ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga, Jumatano wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ‘amekwenda na maji’.  
    Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura imesema kwamba, Kamati ya Ligi imewaondoa marefa watatu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na kuvurunda.
    Mbali na Akrama ambaye ‘Yanga hawana hamu naye’ tangu siku hiyo, wengine ni Paul Soleji wa Mwanza aliyechezesha mechi kati ya Simba na Tanzania Prisons, na mwamuzi msaidizi namba mbili kwenye mechi hiyo Mwarabu Mumbi wa Morogoro, wakati mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga na Simba, Ephrony Ndissa wa Dar es Salaam amepewa onyo.
    Kamishna wa mechi namba 28 kati ya Yanga na African Lyon, Pius Mashera ameondolewa kwenye orodha ya makamishna wa ligi hiyo kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (Pre match meeting) na uwanjani.
    Vilevile Mashera kwenye ripoti yake aliwasilisha malalamiko dhidi ya msimamizi wa kituo cha Dar es Salaam, na kwa vile suala hilo ni la kinidhamu ametakiwa alipeleke kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
    Nayo Simba imepigwa faini ya jumla ya sh. 600,000 kwa kuchelewa kufika kwenye pre match meeting ya mchezo wao dhidi Tanzania Prisons (sh. 100,000) na kwa washabiki wake kuwatupia chupa za maji waamuzi wa mechi hiyo (500,000).
    Pia Kamati ya Ligi imeagiza kuwa kwa vile suala la kipa Shaabani Kado wa Mtibwa Sugar kudaiwa kumpiga kiongozi mmoja wa Ruvu Shooting mara baada ya mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ni la kinidhamu lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: REFA ADUI WA YANGA, SWAHIBA WA SIMBA AENDA NA MAJI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top