• HABARI MPYA

    Tuesday, October 09, 2012

    YANGA WAWASHIKA 'UCHAWI' SIMBA SC KIPIGO CHA KAGERA

    Yanga SC katika moja ya mechi zao, ambazo wanadai eti Simba wanatia mkono

    Na Prince Akbar, Bukoba 
    YANGA SC imesema kwamba wamegundua Simba SC ‘wanatia mkono’ kwenye mechi zao na ndio maana zinakuwa ngumu, ila kuanzia sasa na wao wanaanza ‘fitina’.
    Madai hayo yanakuja, baada ya jana kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wake wa sita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
    “Simba ilituma watu Bukoba watie mkono mechi yetu, sisi tuliwashitukia hao watu baadaye sana, lakini tunashangaa kwa nini wanafanya hivi, wakati sisi tulizungumza nao tukakubaliana haya mambo tuyaache, tucheze mpira, sasa wao wanatuzunguka wanaendeleza mchezo mchafu,”alisema kiongozi Mjumbe mmoja wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, ambaye hakutaka kutajwa jina.
    Mjumbe huyo alisema kwamba wao walijua baada ya makubaliano na Simba kutofanyiana fitina, waliamini mambo hayo hayatakuwapo, lakini baada ya kugundua wenzao wamewageuka sasa na wao wanaanza ‘mchezo huo’.
    “Na sisi sasa tunaanza kuzicheza mechi zao, wakumbuke tu wao ndio walichokoza nyuki, sasa subirini kuanzia mechi yao na Coastal, wakishinda wao wanaume, na pamoja na kuzicheza mechi zao, tunajizatiti katika mechi zetu. Uzuri watu wote wanaowatumia tumekwishawajua, ni wale wale waliokuja Morogoro, na wale wale waliokuja Bukoba. Tumekwishawajua,”alisema Mjumbe huyo.   
    Bao pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, jana liliwapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
    Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC.
    Aidha, hii ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.  
    Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na jana imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
    Katika mechi hiyo ya jana, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
    Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti. 
    Katika mechi zilizochezwa juzi za ligi hiyo, Simba SC ilizidi kujiimarisha kileleni kufuatia ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 29.
    Kiemba alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na mashambulizi ya upande wa kulia.
    Ilikuwa rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
    Nonga naye alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni kiulaini.
    Bao hilo lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
    Kipindi cha pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao mawili zaidi.
    Dakika ya 83 Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango huyo.
    Awali ya hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti.
    Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi tano.
    Katika mechi nyingine za jana, Mgambo imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa Polisi Morogoro 1-0, wakati Toto African imeichapa JKT Ruvu 2-1 na Prisons imelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAWASHIKA 'UCHAWI' SIMBA SC KIPIGO CHA KAGERA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top