• HABARI MPYA

    Monday, October 08, 2012

    YANGA YAPIGWA 1-0 KAITABA

    Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mh  Kanali mstaafu Fabian Massawe akisalimiana na  waamuzi .PICHA ZOTE NA BUKOBASPORTS.COM
    Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mh  Kanali mstaafu Fabian Massawe akisalimiana na wachezaji wa timu ya Kagera sugar

    Timu zote mbili zikimsikiliza mkuu wa Mkoa wa Kagera
    Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mh Kanali mstaafu Fabian Massawe akisalimiana na wachezaji wa timu zote mbili Yanga na Kagera Sugar.Timu zikisalimiana kabla ya mtanange jioni hii
    Kikosi kamili cha Yanga kilichopewa  kichapo na wakata miwa wa Kagera Sukari jioni ya leo.

    Waamuzi wa mpira wa kagera sugar na Yanga (OMARY JUMA - MWANZA, DOMINIQ NYAMSANA - DODOMA-HASSAN ZANI - ARUSHA - CHARLES MBILINYI- MWANZA NA JONESIA LUKYAA-BUKOBA)
    Kikosi cha timu ya Kagera Sukari kilicho ifunga  timu ya Yanga 1-0  kwenye uwanja wa kaitaba mjini hapa

     Kocha wa Kagera Abdallah King Kibadeni (kulia) na wasaidizi wake 
    Kocha wa Kagera Abdallah King Kibadeni akiendelea kufuatilia mtanange kwa makini 

    Bench la Wachezaji wa Kagera Sukari.

    Said Bahanuz aliumia na nafasi yake ikachukuliwa Jerson TegeteSaid Bahanuzi akiendelea kujipoza na maumivu ya nyama za pajani baada ya kupata matatizo

    Meza kuu
    Mkuu wa mkoa wa kagera (katikati) akiwa na Malik Suddy Tibabimale(katibu chama cha mpira BKM) wakifatilia kwa makini mpambano kati ya Kagera Sugar na Yanga.
    Kagera Sugar wakifanya mabadiliko 
    Hadi Half time hakuna timu iliyokuwa imemchungulia mwenzake.
    Wapenzi wa soka Jukwaa la Golani maarufu kama Jukwaa la Balimi.Bench la timu ya Yanga

    Wapenzi wa soka Jukwaa la Golani maarufu kama Jukwaa la Balimi. wakiangaliwa kwa makini Askari wa Ulinzi uwanjani hapo
    Mdau wa Bukobasports.com akichukua matukio tayari kuyarusha live kwenye libeneke la bukobasports.com
    Mashabiki jukwaa kuu 
    Mashabiki jukwaa kuu namuona Mr. Mbelwa mpenzi wa soka akiwa ameshika maji jukwaani na huku akiendelea kucheki mtanange
    Wadau mbalimbali wakifatilia soka na mimi nilikuwa moja wapo baada ya kuonekana hapa 

    Mashabiki 

    Mashabiki 

    Na Prince Akbar, Bukoba
    BAO pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, jioni ya leo limewapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
    Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC.
    Aidha, hii ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.   
    Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na leo imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
    Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti.  
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Omar Juma kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Dominick Nyamsana wa Dodoma na Hassan Zani wa Arusha, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma Abdul, Stefano Mwasyika/nurdin, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi/Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
    Kagera; Andrew Ntala, Jumanne Nade, Salum Kanoni, Amandus Nesta, Benjamin Effe, Malegsesi Mwangwa, Daudi Jumanne, George Kavilla, Enyinna Darlington/Themi Felix, Shijja Mkinna na Wilfred Emmeh/Paul Ngway.
    Katika mechi zilizochezwa jana, Simba SC ilizidi kujiimarisha kileleni kufuatia ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 29.
    Kiemba alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na mashambulizi ya upande wa kulia.
    Ilikuwa rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
    Nonga naye alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni kiulaini.
    Bao hilo lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
    Kipindi cha pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao mawili zaidi.
    Dakika ya 83 Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango huyo.
    Awali ya hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti.
    Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi tano.
    Katika mechi nyingine za jana, Mgambo imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa Polisi Morogoro 1-0, wakati Toto African imeichapa JKT Ruvu 2-1 na Prisons imelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA YAPIGWA 1-0 KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top