• HABARI MPYA

    Sunday, January 06, 2013

    SIMBA YATUPA KETE YA MWISHO MAPINDUZI LEO, JULIO AAHIDI KUJIUZULU TIMU IKIFUNGWA

    Kikosi cha Simba

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    SIMBA SC inarudi dimbani leo katika Kombe la Mapinduzi, kumenyana na Bandari ya hapa katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa kuanzia saa 2:30 usiku.
    Simba SC inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kujihakikishia kutinga Nusu Fainali, kwani hadi sasa ina pointi nne sawa na vinara wa kundi hilo, Tusker FC ya Kenya wenye wastani mzuri wa mabao.
    Kocha Msaidizi wa Simba SC, Jamhuri Mussa Kihwelo ameahidi kujiuzulu leo iwapo timu hiyo itafungwa na Bandari leo.
    Katika mchezo uliopita, Simba SC ilionyesha kuimarika kiuchezaji na kutoa sare dhidi ya timu ngumu, Tusker ya Kenya ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
    Kwenye mchezo huo, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Simba wakitangulia kupata bao dakika ya 18 mfungaji Haruna Moshi Shaaban, maarufu kama Boban au Balotelli wa Bongo kabla ya Tusker kusawazisha dakika ya 39, mfungaji Khalid Aucho.
    Boban alifunga bao tamu sana kwa ufundi wa hali juu akiwa amedhibitiwa na beki ngongoti wa Tusker, Joseph Shikokoti na kuirukia pasi ya Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kuitumbukiza nyavuni.
    Baada ya kufunga bao hilo, Boban aliangukia mkono na kuumia, hivyo hakushangilia bao lake na moja kwa moja alianza kutibiwa na Daktari Cossmas Kapinga wa Simba.
    Baada ya bao hilo, Simba iliongeza mashambulizi langoni mwa Tusker na Boban alikaribia kufunga tena dakika ya 30 kama si shuti lake kutoka nje sentimita chache.
    Aucho alifunga bao lake akiunganisha krosi ya Jeremiah Bright kutoka upande wa kushoto wa Uwanja.
    Baada ya hapo, timu zilianza kushambuliana kwa zamu hadi refa Ramadhani Kibo alipopuliza kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza.
    Kipindi cha pili timu zote zilirudi vizuri na kucheza kwa umakini wa hali ya juu, jambo ambalo lilisababisha dakika 90 zimalizike zikiwa zimefungana 1-1.
    Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kuwa kile kile kilichotoa sare ya 1-1 na Tusker; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Shomary Kapombe, Komabil Keita, Jonas Mkude, Haroun Athumani, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
    Julio kushoto akiwa na Kocha Mkuu, Patrick Liewig. Ameahidi kujiuzulu timu ikifungwa

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA YATUPA KETE YA MWISHO MAPINDUZI LEO, JULIO AAHIDI KUJIUZULU TIMU IKIFUNGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top