Bingwa 2009 Man.United
Mazowea ya Ferguson kila mwaka
MWALI bado kafichwa kwa sababu mwenye dau
kubwa bado hajajulikana, japokuwa ni kati ya wababe wawili wa Manchester -
Manchester City na Manchester United.
Timu hizi mbili zina pointi 86, lakini City
wana mabao mengi manane kuliko United.
Kwa kuzingatia hayo, mechi muhimu zaidi
Jumapili hii ni ile inayozikutanisha Manchester City na Queen Park Rangers
(QPR), mchezo unaofanyika Etihad, nyumbani kwa City mbele ya washabiki wake.
Mechi nyingine inayotia wadau matumbo joto
ni ile ya Manchester United na Sunderland, United safari hii wakichezea
ugenini.
Ili City watwae ubingwa wanatakiwa kuwa na
matokeo kama ya United au mazuri zaidi. Kwa kifupi ni kwamba, City wakishinda
kuna uwezekano mkubwa wa kutangazwa wafalme wa soka wa England.
Ni katika hali hiyo Kocha Mkuu wa
Manchester United, Sir Alex Ferguson anasema wao wanaombea litokee jambo la
'kijinga' dhidi ya jirani zao (Manchester City) ili wanyakue tonge mdomoni
mwao. Kwamba wao United watatekeleza wajibu wao kujitahidi kushinda mechi yao,
lakini kulipata kombe itategemea nyumba ya jirani.
Lakini ikumbukwe kwamba vijana hao wa
Roberto Mancini katika msimu wote wamepoteza pointi mbili tu katika uwanja wao
huo wa Etihad, yaani wameshinda mechi zote isipokuwa mbili tu walizotoka sare.
Ndiyo maana washabiki wao wengi wana
matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa walioupata mara ya mwisho mwaka 1968.
Wanachotegemea dhidi ya QPR ni ushindi tu.
QPR wananolewa na kocha wa zamani wa City,
Mark Hughes aliyetupiwa virago Desemba 2009 baada ya kushinda mechi mbili tu
kati ya 11 City walizocheza mfululizo. Kocha huyo pia ameichezea United na
Ferguson anamtegemea 'amsaidie kuiangamiza City'. Kwa ujumla timu mbili hizi za
Manchester zinatarajiwa kuibuka na ushindi kwenye mechi zao hizi za mwisho.
Ligi ya Mabingwa Ulaya
Moja ya mambo yanayotafutwa kwenye mbio za
Ligi Kuu ya Uingereza ni nafasi za timu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa minajili ya Uingereza wakati huu,
panaweza kuwapo nafasi moja au mbili, wakati timu zinazowania ni Arsenal wenye
pointi 67,
Tottenham waliojikusantia pointi 66 na
Newcastle waliovuna pointi 65.
Mechi muhimu katika kuamua hili ni kati ya
Everton na Newcastle; Tottenham Hotspur dhidi ya Fulham na West Brom
wanaoikaribisha Arsenal.
Hali ilivyo ni kwamba hatima ya Arsenal imo
mikononi mwao wenyewe, kwa maana kwamba wanachotakiwa ni kushinda tu ili kufuzu
moja kwa moja, bila kusubiri matokeo ya mechi nyingine. Ushindi utawahakikishia
kubaki nafasi ya tatu wanayoshikilia
Hata hivyo, ikiwa Arsenal watatoa sare
dhidi ya Baggies, wanaweza kuvukwa na kutupwa nafasi ya nne ikiwa Tottenham
watawafunga Fulham.
Maana yake ni kwamba Washika Bunduki hao wa
London hawatakuwa na chaguo zaidi ya kuingia kwenye mechi za mchujo ili kufuzu,
huku Spurs wakisonga moja kwa moja kwenye mashindano hayo makubwa ya Ulaya.
Ikiwa Arsenal watachezea kichapo nyumbani
kwa West Brom, ni dhahiri pia watakuwa wamejiweka pabaya, kwa sababu wataweza
kupitwa na Spurs watakaohitaji sare tu
ikiwa Arsenal itafungwa mabao mawili au
zaidi. Arsenal pia watapitwa na Newcastle inayonolewa na Alan Pardew, ikiwa
watawafunga Everton.
Vinginevyo ni kwamba Tottenham wakishinda
mechi yake tu itakuwa imejihakikishia kupata nafasi ya nne na sare pia inaweza
kuitosheleza ikiwa Newcastle hawatawafunga Everton.
Kwa upande mwingine, ili Newcastle waweze
kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lazima wawafunge Everton na kuomba ama
Arsenal au Tottenham wasishinde mechi zao. Ikiwa hizo tatu zitatokea, basi
Newcastle itamaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tatu.
Hata hivyo, ikiwa Chelsea itatwaa Kombe la
Mabingwa Ulaya kwenye fainali dhidi ya Bayern Munich mjini Munich Mei 19 mambo
yatabadilika Uingereza, kwa sababu timu itakayoshika nafasi ya nne kwenye EPL
mwaka huu haitakuwa na nafasi kwenye ligi hiyo tena.
Badala yake, timu hiyo itaingia kwenye Ligi
ya Europa pamoja na watakaomaliza ligi wakiwa nafasi ya tano, kwani timu
inayotwaa kombe hilo inashiriki msimu unaofuata kulitetea.
Katika mazingira haya, Arsenal watatakiwa
kutumia vyema nguvu na fursa kuwamaliza West Brom, kwani kwao msimu ni kama
umeshaisha tu, hawana kikubwa cha kupata wala kupoteza.
Spurs wanaelekea pia kwamba watawafunga
Fulham, na maana ya haya ni kwamba kuna kila dalili za Newcastle kuachiwa
simanzi bila kupenda.
Pengine Bayern watalitwaa kombe la Ligi ya
Mabingwa, na kwa kufanya hivyo mazingira ya Ligi kuu ya England na ushiriki wa
msimu ujao kimataifa kutoathiriwa.
0 comments:
Post a Comment