![]() |
Torres, atafan ya maajabu kesho? |
HAYAWI hayawi, sasa hamekuwa- The Blues, Chelsea wanashuka dimbani
Jumamosi katika fainali Ligi yaa Mabingwa Ulaya, dhidi ya wenyeji Bayern Munich.
Chini ya kocha wa muda, Roberto Di Matteo, Chelsea wana kazi
ngumu bado, kwani watakuwa Allinz Arena, nyumbani kwa Bayern Munich,
wakikabiliana nao kwenye fainali.
Kama ndoto vile, katika nusu fainali, Chelsea iliwashangaza
wengi, kwa kuisambaratisha timu bora Ulaya na duniani, Barcelona.
Fainali ya wikendi hii ni wazi itakuwa ngumu kwa timu zote,
huku Chelsea wakiwa wameshajijenga kisaikolojia na kujiamini kwamba wanaweza.
Hata kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes anaamini kwamba,
kwa timu yake kucheza nyumbani, ina nafasi kidogo tu juu ya Chelsea, anaosema
ni hatari.
Ni mchezo unaosubiriwa na wengi, utakaokusanya mashabiki
wengi katika uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 66,000 katika mechi za
kimataifa.
Chelsea wanaingia uwanjani wakijua ugumu wa mechi yenyewe,
licha ya ukweli wa kuifunga Barcelona, kwa sababu Bayern Munich ni timu ngumu
popote inapochezea, lakini pia itakuwa ikishangiliwa na maelfu ya mashabiki
wake.
Bila shaka kocha Di Matteo atatathmini na kutumia kila
mwanya, iwe wa kisoka au kisaikolojia kwa ajili ya kuwaweka wachezaji wake
kwenye nafasi nzuri.
Wanatakiwa kuondoa hofu na kuweka kando uzito wa mazingira
ya mchezo huo wa ugenini ili kutwaa zawadi kubwa zaidi ya soka katika bara la
Ulaya.
Si rahisi hata hivyo, kwa Chelsea kurudia mbinu walizotumia
Liverpool walipojikuta katika mazingira ya aina hii mwaka 1984 walipokabiliana
na AS Roma kwenye uwanja wa Stadio Olimpico.
Katika mechi hiyo iliyofanyika Roma, Italia nyumbani kwa AS
Roma, Liverpool waliwabana wenyeji wao na kutoka sare ya bao 1-1 na baadaye
kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 walipopigiana mikwaju ya penalti.
![]() |
Bastian Schweinsteiger, tegemeo la Bayern katika safu ya kiungo. |
Liverpool katika mechi hiyo hawakubabaishwa na mashabiki wa
AS Roma, wakaenda sambamba na nyimbo walizokuwa wakiimba na kuzichukulia kana
kwamba ni za dimbani kwao Anfield.
Taratibu wakawachota na kuwanyamazisha wapinzani wao
nyumbani kwao.
Mark Lawrenson wa Idara ya Michezo ya BBC alicheza kwenye
fainali hiyo na bado anakumbuka mambo yalivyokuwa hata leo.
“Kwenye chumba cha kubadilishia nguo tulicheka sana tukiwa
na baadhi ya watu mashuhuri (kama Kenny Dalglish na Ian Rush).
“Tulishazunguka uwanjani kukabiliana na kuzoea mazingira
yasiyokuwa mazuri kwetu. Hilo lilikuwa wazo la Graeme Souness (mchezaji wa
Liverpool enzi hizo),” anakumbukia Lawrenson.
Anasema kwamba kabla ya mchezo pia walipata fursa ya kuimba,
kuonyesha jinsi walivyojiamini, kocha wa AS Roma, Nils Liedholm aliyekuwa
akikamilisha kuwapanga wachezaji akapigwa butwaa, huku wachezaji wake
wakionekana kutoamini.
Lawrenson anasema ikiwa Chelsea wanaweza kupata kitu cha aina
hiyo kitakachowapa moyo na kuinua morali, ni muhimu kufuata nyayo zao, kwa
sababu hatimaye Liverpool walifanikiwa.
“Wasikubali Bayern wawape mashabiki wao kitu cha kushangilia
mapema hata kidogo. Mchezo unatakiwa uwe umetulia kama maji ya mtungi, ikiwa
hivyo, natabiri mambo yatakuwa mazuri kwa Di Matteo,” anasema.
Alan Hansen, mchezaji mwingine aliyekuwa akicheza nafasi ya
ulinzi Liverpool sambamba na Lawrenson, naye anakumbuka jinsi walivyoibuka na
kuanza kuimba wakijipa moyo ugenini.
“Lazima walituangalia (AS Roma) na kudhani tumeingiwa
wazimu, lakini ukweli ni kwamba kilikuwa kiashirio cha umoja na ushirikiano
tuliokuwa nao. “Tulishikamana kabisa, na hicho ndicho Chelsea wanachotakiwa
kufanya wanapocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa nyumbani kwa wapinzani wao.
Wawe ndio maneno ya mwisho kwa kila mmoja – washikamane maana bila hivyo
mnakuwa si chochote kwenye michezo hii.
“Yaweza ikaonekana kana kwamba mazingira si ya haki kwa
Chelsea, lakini Chelsea siku zote walikuwa wanajua ni wapi fainali ingeenda kuchezwa.
“Unaweza pia kufikiria kwamba kwa kucheza kwenye uwanja wao
wa nyumbani, shinikizo litaongezeka kwa Bayern, lakini ngoja niseme, shinikizo
zinakuwapo kila mahali,” anaeleza mkongwe huyo wa soka.
Ukiachilia mbali suala la kucheza nyumbani au ugenini enzi
hizo, AS Roma ilipewa nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu ilikuwa imeahidiwa
kitita kikubwa mara 10 ya Liverpool.
Liverpool walipata £6,000 wakati AS Roma walikuwa wapate
zawadi ya £64,000
Pengine mtu mpweke zaidi duniani usiku huo atakuwa John
Terry. Huyu tamaa yake kubwa ilikuwa kutumia maarifa yote ili washinde, lakini
hataruhusiwa kucheza kutokana na kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo dhidi ya
Barcelona.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba katika mechi ya nusu fainali ya
pili dhidi ya Barcelona, Chelsea walicheza muda mrefu zaidi bila Terry, tena
wakiwa 10 dhidi ya 11 wa adui zao na bado wakavuka.
Zaidi ya hapo ni kwamba Chelsea itakuwa na wachezaji wake
mahiri kama Frank Lampard, Ashley Cole, Didier Drogba na kipa aliyefanya kazi
ya ziada kwenye mechi zote zilizopita, Petr Cech.
Wengine ambao wamezuiwa kucheza kwa upande wa Chelsea ni
Branislav Ivanović, Raul Meireles na Ramires.
Habari njema pia za kuwapo wachezaji Gary Cahil na David
Luiz zinawaweka wachezaji wenzao, kocha na mashabiki kujawa imani zaidi kwamba
wataweza kufanya vizuri.
Hata hivyo, Bayern Munich ni timu ya kuangalia vizuri, kwa
sababu ni kikosi kilichojipanga na kinachocheza kwa nguvu na akili.
Wachezaji wake wanaweza kuwatia wehu Chelsea kwa kuwatembeza
uwanja mzima, wakiwavuta huku na kule, hata kama Chelsea wangependa kutumia
mtindo wa kulinda zaidi lango lao.
Walifanikiwa kufanya hivyo baada ya kupata bao la kwanza la
kushitukiza lililowaacha wengi midomo wazi katika nusu fainali ya kwanza dhidi
ya Barcelona.
Chelsea walirudia aina hiyo ya mchezo kwenye Uwanja wa Camp
Nou jijini Madrid, Hispania, huku wakifanya mashambulizi ya kushitukiza, kama
yaliyowapatia mabao kupitia kwa Ramires Santos do Nascimento na la pili dakika
za lala salama kupitia kwa mkongwe aliyesahaulika, Fernando Torres.
Katika hili, Chelsea wanatakiwa kuwa makini na Bayern
Munich, kwa sababu inao wakongwe wanaoweza kuwa tishio kubwa kwa klabu hiyo ya
London na kuwafanya waondoke Munich kwa aibu usiku huo.
Hao ni pamoja na Franck Ribery na Arjen Robben wenye uwezo
mkubwa wanapokuwa dimbani, wakisaidiwa na wachezaji wa nyuma ambao wamekuwa
wakihakikisha kipa wao hasulubiwi.
Yote kwa yote, kocha Di Matteo atakuwa ameshasoma na kupanga
mbinu za kukabiliana nao, huku wachezaji wakisema kama waliwaweza Barcelona,
kipi kitashindikana kwa Bayern?
Labda hilo ndilo linaloangaliwa pia na kocha wa Bayern
Munich, Jupp Heynckes, ambaye atakuwa uso kwa uso na Di Matteo, kila mmoja
akiwapanga wachezaji wake ili hatimaye acheke wa mwisho.
Kama ni uzoefu, pengine ni vigumu kupata kocha wa
kumfananisha na Heynckes.
Huyu alianza ukocha wakati Di Matteo hajaanza hata kucheza
mpira wa kulipwa. Ni huyu aliyeiwezesha Real Madrid kutwaa ubingwa wa Ulaya
mwaka 1998.
Licha ya uzoefu na mafanikio yake mengi, kocha huyo mwenye
umri wa miaka 67 anasema anaihusudu Chelsea inavyojituma tangu Di Matteo
alipoteuliwa kuwa kocha wa muda Machi mwaka huu.
Haoni sababu ya kubweteka, kwa vile anaamini Chelsea imekuwa
ikibadilika kuendana na matakwa ya mazingira kwa kila mechi, na kwa hilo
imefanikiwa mara kadhaa.
“Unaona Chelsea wanaweza kucheza mifumo tofauti. Walicheza
tofauti kabisa walipokabiliana na Benfica (ya Ureno, kwenye robo fainali)
ikilinganishwa na walivyocheza dhidi ya Barcelona.
“Natarajia kwamba Chelsea itakuwa tofauti kidogo
(itakapocheza na Bayern Munich) na ilivyokuwa ikicheza na Barcelona. Kwa hakika
timu hii imekuwa ikipita kwenye kipindi kizuri katika wiki zilizopita.
Wanacheza soka nzuri zaidi na yenye mafanikio," Anasema
Heynckes anayetafuta rekodi ya kuwa kocha wa nne kupata kombe hilo akiwa na
timu tofauti.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi
aliyechukua hatamu za Bayern Munich kwa mara ya tatu kipindi kilichopita cha
majira ya joto, anawaheshimu wachezaji wa Chelsea.
“Wana wachezaji uzeofu mkubwa katika timu yao na ni wazi
kwamba maveterani hao, wachezaji walioichezea Chelsea kwa muda mrefu wanataka
kusinda kitu fulani kikubwa. Hiyo ni hatari kubwa kwetu.
“Mchezo utakuwa wazi na nafasi za timu kushinda ni nusu kwa
nusu, lakini huenda tukafaidika kidogo kwa kucheza hapa nyumbani,” anasema kwa
matumaini mtaalamu huyo wa soka.
Pamoja na kufaidika kwa kuchezea nyumbani, Heynckes anajua
kwamba mechi hii muhimu inatoa fursa kwake kuandika historia kwa timu aliyoipa
ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mara mbili mfululizo – 1988/89 na
1989/90.
“Ni jambo la kipekee kucheza fainali kwenye uwanja wenu, ni
kitu kisichokuwa cha kawaida, kwa hiyo ushindi kwetu litakuwa jambo kubwa
sana,” anasema.
Hata hivyo, kitu kinachomuumiza kichwa mkongwe huyo
aliyepata kuwa VfL Borussia Mönchengladbach ni jinsi ya kuziba pengo la nyota
wake watatu ambao hawatacheza Jumamosi hii.
Hao ni Holger Badstuber, David Alaba na Luiz Gustavo. Kocha
huyo anasema angefurahi zaidi ikiwa wachezaji wote muhimu kwa timu hizo mbili
wangekuwa dimbani, ili wachuane ipasavyo.
Hivi sasa Kombe la Ubingwa wa Ulaya halina mwenyewe, baada
ya Barcelona kulitema walipotandikwa na Chelsea kwa uwiano wa mabao 3-2.
Barcelona walitwaa kombe hilo Mei 28, 2011 katika Uwanja wa
Wembley, Uingereza, baada ya kuwafunga Manchester United kwa mabao 3-1.
Barcelona walitawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa, na mabao
yao yalifungwa na Pedro RodrÃguez, Lionel Messi na David Villa.
Wayne Rooney ndiye alifunga bao la United na kuzifanya timu
kwenda mapumziko zikiwa sare ya mabao 1-1.
Jumamosi hii, wadau wa Chelsea wana hamu ya kuiona timu yao
ikitwaa kombe hilo na kujiwekea heshima kote barani Ulaya.
Licha ya kombe na zawadi, Di Matteo anaangaliwa kwa karibu,
kwa sababu uamuzi wa nani awe kocha mpya utatolewa baada ya fainali hizi.
Chelsea haikumaliza ligi mahali pa kuweza kujidai wala
kufuzu uwakilishi wa Ulaya, kwani iliishia nafasi ya sita, ikijifariji kwa
kutwaa Kombe la FA na kufika fainali hii muhimu.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chelsea, Ron Gourlay alisisitiza wiki
moja kabla ya mechi hii kwamba hatimaye ya Di Matteo haingeamuliwa kabla ya
mashindano hayo makubwa zaidi barani Ulaya kumalizika.
Pengine Di Matteo hajafanya vya kutosha kiasi cha
kukabidhiwa mikoba ya klabu hiyo kongwe moja kwa moja, na uamuzi wa mwisho
waweza kutoka kwa mmiliki wa klabu, bilionea wa Kirusi, Roman Abramovic.
Huenda fainali hii ikawa nafasi ya mwisho kwa baadhi ya
wachezaji wakongwe wa klabu hiyo kama Didier Drogba kuichezea, japokuwa Gourlay
anasema mazungumzo kuhusu mkataba wake unaomalizika majira haya ya joto
yanaendelea.
Licha ya kunyakua Kombe la FA kwa kuwafunga Liverpool,
Chelsea ilikuja kufungwa na wababe hao wa Anfield wiki iliyofuata kwa mabao 4-1
kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England (EPL) na kutia uchachu kwenye tamu ya
ushindi wao wa awali.
Mtaliano Di Matteo alipewa nafasi ya muda ya ukocha baada ya
kufukuzwa kwa kocha kutoka Ureno,
Andre Villas-Boas, maarufu kama AVB, ambaye matokeo ya
mfululizo katika siku zake za mwisho hayakuwa yakiridhisha.
Alipoondolewa, wakuu wa Chelsea walisema walidhani hatua
hiyo ilikuwa muhimu, kwa sababu walitaka kumaliza EPL kwenye nafasi nzuri.
Lakini pia walikuwa wakizingatia ushiriki wao kwenye
michuano ya Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
0 comments:
Post a Comment