WIKI hii, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Danny Davis
Rwanda alichangia habari niliyoandika kuhusu mshambuliaji wa Simba kutoka
Ghana, Daniel Akuffor. Habari ilikuwa inamnukuu kocha wa Simba, Profesa Milovan
Cirkovick akisema kwamba Mghana huyo kwa sasa hapangwi katika kikosi cha kwanza
kwa sababu wanaopangwa wanamzidi uwezo.
![]() |
Na Mahmoud Zubeiry |
Mrwanda, akiwa miongoni mwa watu wa awali kabisa kuchangia,
akaandika; “Tatizo 20 percent kaka”akimaanisha tatizo ni asilimia 20.
Baadaye niliwasiliana binafsi na Mrwanda kumuomba
anifafanulie juu ya alichochangia, lakini akagoma.
Hata hivyo, kwa mtazamo wa wengi ni kwamba, hivi sasa Simba
ili ucheze lazima ukate asilimia 20. Ya nini? Sijui!
Hii si mara ya kwanza mimi kusikia malalamiko kama haya
kutoka kwa wachezaji, ambao wapo katika wakati mgumu Simba- wakidai kuna
viongozi wanapeleka wachezaji wao kwenye timu hiyo hata kama hawana uwezo, ili
mradi tu wanakata asilimia 20.
Wakati fulani Yanga ilipokuwa chini ya kocha Mserbia, Profesa
Dusan Savo Kondic kulikuwa kuna kashfa kama hii ya asilimia 20, ambayo ilihusu
fedha za usajili na mishahara. Yussuf Manji, mfadhili wa Yanga, aliifanyia kazi
vizuri kashfa hiyo na alipogundua akachukua hatua, watu walipoteza kazi
Jangwani.
Wachezaji walioachwa Simba baada ya msimu uliopita wengi wao
wanalalamikia hiyo asilimia 20 na baada ya kuwa malalamiko ya chini chini,
hatimaye sasa yanaanza kuwekwa hadharani.
Mrwanda anayelalamikia asilimia 20, ni ambaye alikuwemo
kwenye kikosi cha Simba cha msimu huu, akisajiliwa tena kutoka Vietnam
alipokuwa anacheza soka ya kulipwa, lakini akaachwa dakika za mwishoni kabla ya
kufungwa kwa dirisha la usajili.
Nilijiuliza, kweli Mrwanda alikuwa katika kiwango cha kuachwa
Simba? Mrwanda yule ambaye Simba ilimsajili ikimgombea dhidi ya mahasimu wao wa
jadi, Yanga?
Mrwanda yule ambaye alitokea benchi kwenye Fainali ya Kombe
la Urafiki, Simba ikiwa nyuma kwa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC na kwenda
kusababisha penalti iliyoipa Simba bao la kusawazisha na hatimaye kutwaa Kombe
hilo kwa mikwaju ya penalti?
Yakawa yanaibuka majibu ya pembeni, eti Mrwanda kiburi sana
ameshindwana na kocha, yaani Milovan. Labda!
Lakini sasa Mrwanda anafunguka, baada ya kimya kirefu anasema
tatizo ni asilimia 20. Amri Kiemba amepata tabu sana kupata namba kwenye kikosi
cha kwanza cha Simba msimu huu na sasa anaisaidia sana timu.
Amri alirudishwa uwanjani, baada ya kuonekana kabisa timu ina
tatizo katika nafasi ya kiungo wa ulinzi- hakukuwa na jinsi amerudishwa na
anaonyesha umuhimu wake kwa kuibeba sana timu na kuwaacha ‘visokorokwinyo’
vichwa chini kwa fedheha.
Bado najiuliza, mshambuliaji Abdallah Juma ‘Dullah Mabao’ kwa
nini hapangwi katika kikosi cha kwanza cha Simba, wakati dogo alionyesha uwezo
mkubwa sana kuanzia kwenye michuano ya Kombe la Urafiki hadi Kombe la Kagame.
Huyu kijana amekuwa akipigwa mizengwe tangu wakati anataka
kusajiliwa akitokea Ruvu Shooting, lakini Mungu wake alimsimamia. Ila sasa
hachezi na haumwi, kwa nini?
Simba ni bora sana na ndio maana ni mabingwa wa Tanzania na
klabu yenye rekodi nzuri zaidi katika michuano ya Afrika- lakini inaweza kuwa
bora zaidi iwapo baadhi ya mambo yanayokwenda kinyume na maadili yataondolewa
katika klabu hiyo.
Yupo mtu mmoja aliwahi kuniambia; “Huyu Paul Ngalema hata awe
mzuri vipi, hawezi kucheza Simba, kwa sababu mwenye namba yake mjomba wake ni
kiongozi wa Simba na ndiye aliyemsaidia kuingia Simba, baada ya kufukuzwa
Yanga,”.
Japokuwa nilimpuuza kwa kuwa naamini viongozi hawawezi
kumuingilia kocha, lakini kwa kauli hii ya Mrwanda sasa naanza kupata shaka
kuna mambo yaliyo kinyume cha maadili yanaendelea Simba SC.
Naamini ndani ya Simba hakuna mtu mwenye nguvu kuliko Simba
yenyewe- hivyo ipo haja kwa uongozi wa klabu hiyo hivi sasa ukayafanyia
uchunguzi madai haya, ili kama yana ukweli wowote hatua ichukuliwe, ili
kuisafisha klabu.
Hivi kweli leo, Mrwanda na Akuffo waitwe kufanya majaribio
timu moja, nani atafuzu jamani au turudie mara mbili mbili uchezaji wa Abdallah
Juma na huyo Mghana, nani anastahili kutokea benchi kwenda kuiongezea nguvu
timu japo kwa dakika 20 za mwisho?
Katika uongozi, kama kuna jambo la msingi sana, kwanza ni
maadili. Kama viongozi wanakuwa siyo waadilifu basi timu haitakuwa na misingi
imara hata kidogo. Hivyo basi, ipo haja uongozi wa Simba, kuifanyia kazi kashfa
hii ili kama ni kweli ipo, hatua zichukuliwe.
Wakati fulani niliwahi kufanya mahojiano na Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akaelezea mfumo mzima wa
utendaji wa Kamati yake- kwamba yenyewe inapokea mapendekezo ya Kamati ya
Ufundi na benchi la ufundi juu ya usajili na kutekeleza jukumu la kusajili.
Lakini Hans Poppe akasema kuna wachezaji ambao wamekuwa
wakiingia kinyume cha utaratibu uliowekwa na bila shaka tatizo linaweza kuwa
linaanzia hapo.
Uadilifu ni tatizo kubwa sana katika soka yetu, watu
wanaingia madarakani na miili kama ya wanariadha wa mbio ndefu, lakini baada ya
miezi sita wanafutuka kama warusha matufe. Mungu ‘amrehemu’ hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, wakati wake alisimamia uadilifu kikamilifu na
alichukua hatua kali dhidi ya viongozi waliokosa uadilifu- si tunakumbuka enzi
zile za staafisha kwa manufaa ya umma?
Leo ni miaka 13 tangu tumpoteze baba wa taifa letu,
tunaishuhudia Tanzania tofauti, iliyokithiri utovu wa maadili na uzalendo,
kwenye soka ndiyo balaa! Wito kwa Simba SC, wamuenzi mwalimu Nyerere kwa
kupambana na hawa 20 Percent, ili kusafisha hadhi ya klabu yao!