• HABARI MPYA

    Friday, October 05, 2012

    YANGA SC WAIFUATA KAGERA SUGAR KESHO

    Basi la Yanga

    Na Mahmoud Zubeiry
    BAADA ya kulazimisha sare ya bila kufungana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC Jumatano, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga inatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kwenda Bukoba kwa ajili ya mchezo wake wa sita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Kagera Sugar Jumapili.
    Yanga leo itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam na baada ya hapo itakuwa tayari kwa safari ya Bukoba na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, kwani baada ya kucheza na Kagera, itacheza na Toto African mjini Mwanza.
    Katika mechi nne za awali ilizocheza, Yanga imefungwa moja, sare mbili na kushinda mbili, hivyo kujikusanyia pointi nane, ikizidiwa pointi tano na wapinzani wao wa jadi, Simba wanaoongoza ligi hiyo.
    Jumatano Yanga ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao hao wa jadi, Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
    Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.  
    Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili.
    Simba walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za uhakika na kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na kuzinduka baada ya kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
    Pasi zao zilikuwa nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira kirahisi, wanazidiwa nguvu na wapinzani wao katika kugombea mipira na hata mashambulizi yao hayakuwa ya mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi.
    Katika kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.    
    Kabla hata ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha Mholanzi Ernie Brandts alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili kuimarisha safu ya kiungo, ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa na Mserbia, Milovan Cirkovick.
    Kipindi cha pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts akimtoa kiungo Nizar Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu, ambaye alikwenda kuongeza nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
    Angalau, kipindi cha pili Yanga walionekana kucheza vizuri na kupeleka mashambulizi yenye uhai langoni mwa Simba, ingawa safu imara ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi ilikuwa kikwazo.
    Katika dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.
    Pamoja na Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na mashambulizi yalikuwa ya pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu mchezo na maamuzi yake mengi yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’ alipomchezea rafu mbaya beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
    Hakumchukulia hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
    Alipoingia Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu Twite akahamia katikati kucheza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake ilicheza vizuri na anajivunia. Alisema Yanga imeimarika tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu msimu huu itakuwa ngumu.
    Kwa upande wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini baadaye walitulia na kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani, unaweza kuona rafu na kadi nyingi,”alisema Brandts.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAIFUATA KAGERA SUGAR KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top