![]() |
Sunzu akitibiwa na daktari wa Simba, Dk Cossmas Kapinga katika moja ya mechi za Ligi kuu mzunguko wa kwanza msimu huu. |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. ametemwa kwenye kikosi cha Simba
SC kutokana na kuomba yeye mwenyewe na uongozi wa klabu hiyo kuridhia.
Habari za
ndani kutoka Simba SC, zimesema kwamba Sunzu alifika Dar es Salaam na
kuzungumza na viongozi wa klabu hiyo, akiomba aachwe kwani hawezi kucheza kwa
sasa kutokana na matatizo ya kiafya yanayomkabili.
“Sunzu bwana
amekuja mwenyewe kuomba na sisi baada ya kuona hali yake, kwa kweli kibinadamu
tumemkubalia aende,”kilisema chanzo chetu kutoka Simba SC.
Sunzu
alisajiliwa Simba SC Julai 25 mwaka jana, akitokea El Hilal ya Sudan akisaini
mkataba wa miaka miwili kwa dola za Kimarekani 35,000 na mshahara wa dola
3,000.
Kutemwa kwa
Sunzu kunafanya idadi ya wachezaji wa kigeni waliotemwa Simba kufika watatu,
baada ya awali kutemwa beki Paschal Ochieng kutoka Kenya na mshambuliaji Daniel
Akuffo kutoka Ghana.
Simba
inamrejesha kikosini Mussa Mudde na kusaini Waganda wapya wawili, kipa Hamza
Muwonge na mshambuliaji Brian Umony, ambao wataungana na Mganda mwenzao kwenye
klabu hiyo, Emmanuel Okwi kufanya idadi ya wageni watano kwa mujibu wa kanuni
za Bara.