![]() |
Okwi |
Na Frank Sanga
SIMBA
imemuuza mchezaji wake wa Uganda, Emmanuel Okwi kwa timu ya Etoile du Sahel ya
Tunisia kwa kitita cha Dola za Marekani 300,000 (Sh 480 milioni).
Ni jambo la
faraja kuona kuwa klabu za Tanzania zinaweza kunufaika kutokana na biashara ya
wachezaji na hata kufikia uwezo wa kuuza wachezaji kwa bei kubwa kiasi hicho.
Si faraja
kwa Simba tu, lakini ni jambo zuri kwa mchezaji mwenyewe kwani amepata
changamoto mpya ya maisha ikiwa ni pamoja na kupata mshahara mzuri tofauti na
aliokuwa akiupata Simba.
Katika
mkataba mpya wa Simba, Okwi alitakiwa awe analipwa dola 3,000 (sh 4.8 milioni)
kwa mwezi, lakini akiwa Etoile du Sahel atalipwa dola 15,000 (Sh 24 milioni)
kwa mwezi kitu ambacho ni mafanikio makubwa kwa maisha ya mchezaji mwenyewe.
Simba
imemuuzwa mchezaji huyo huku ikiwa ni miaka miwili tu tangu iwauze Mbwana
Samatta na Patrick Ochan kwa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo kwa thamani ya dola 200,000 (Sh 300 milioni).
Kilichotusukuma
kuandika maoni haya ni kuhoji jinsi fedha za kuwauza wachezaji hao
zinavyotumika. Ukiuliza jinsi fedha za kuwauza Samatta na Ochan zilivyotumika
utapewa maneno mengi ambayo hayana kichwa wala miguu.
Tunahoji
hivyo kwa sababu tayari tumesikia kuwa baadhi ya viongozi ndani ya Simba
wameibuka na kudai kuwa wanaidai klabu hiyo fedha. Sisi tunadhani hii ni aibu
kubwa kwa viongozi wa Simba kutaka kutumia fedha za mauzo ya Okwi kwa ajili ya
kulipana madeni.
Mashabiki wa
Simba watataka kuona fedha hizo zikifanya jambo fulani zuri iiwezekana hata kujenga
hatua za mwanzo za uwanja au kitega uchumi chochote ambacho kitaonekana mbele
ya kila mmoja.
Lakini
tunapata wasiwasi kama hayo yatafanyika na hasa tukikumbuka kuwa fedha za
Samatta na Ochan hazikufanya lolote zaidi ya viongozi kudai kuwa walitumia
kusajili wachezaji wengine.
Ni jambo
ambalo linatia aibu na linachukiza kuona kuwa klabu zinapata fedha kwa kuuza
wachezaji, lakini matumizi yake yanazua maswali mengi huku viongozi wakilipana
kwa madai kuwa wanaidai klabu hiyo.
Ni wakati
sasa, wanachama wa Simba kuamka na kuhoji jinsi fedha za kuwauza wachezaji
zinavyotumika katika klabu hiyo ya Msimbazi badala ya kukaa kimya na kuwaacha
viongozi wakilipana madeni.
Viongozi wa
Simba nao wanapaswa kujua kuwa fedha hizo si za kwao, ila ni mali ya klabu
ambayo inaundwa na wanachama na wadau mbalimbali hivyo panapokuwa na keki kama
hiyo ni vizuri ikagawiwa kwa wote.
Unaweza vipi
kugawa fedha hizo kwa wanachama? Ni jambo jepesi ni kujenga uwanja ambao
utaifanya klabu hiyo kuwa na uwanja wake tofauti na sasa ambapo imekuwa
ikifanya mazoezi katika viwanja vya kubangaiza.
Inatia
hasira kuona baadhi ya viongozi wamegeuza klabu kuwa mali zao binafsi na
kuzifanya kuwa vitega uchumi kwa ajili ya kuendeleza familia zao badala ya
kuzifaidisha klabu zenyewe. (Kutoka gazeti la Mwanaspoti leo).