![]() |
Ngalema akiugulia maumivu jana |
Na Mahmoud Zubeiry, Arusha
BEKI tegemeo wa kushoto wa Simba SC, Paul Ngalema hatacheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwishoni mwa wiki dhidi ya Recreativo de Libolo ya Angola, kutokana na maumivu ya goti.
Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Ngalema ameumia goti la mguu wa kushoto katika mchezo wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa.
Kapinga amesema, Ngalema ameondoka leo Arusha kurejea Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi juu ya maumivu yake, na baada ya hapo atajua rasmi atakuwa nje kwa muda gani.
Beki huyo wa kushoto, Ngalema alitoka uwanjani dakika ya 23 jana, baada ya kuumia wakati Simba ikiongoza kwa bao 1-0 kabla ya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.
Simba inabaki Arusha kwa siku mbili zaidi hadi Jumatano itarejea Dar es Salaam kufanya maandalizi ya mwishoni kabla ya kuivaa Libolo, ambayo tayari iko Dar es Salaam.
Simba SC imeweka kambi katika hoteli ya Bridge Stone na itafanya mazoezi mjini hapa, leo, kesho na keshokutwa kabla ya Jumatano kurejea Dar es Salaam.