![]() |
Chuji 24; Ubingwa wa 24 |
Na Mahmoud Zuberiy, IMEWEKWA MEI 12, 2013 SAA 8:45 MCHANA
ATHUMANI Iddi Athumani ‘Chuji’ kwamba amesema sababu ya kuchagua jezi namba 24 msimu huu ni alijua klabu yake, Yanga itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kuzidi kuvunja rekodi zake kwa kufikisha taji la 24 la ligi hiyo.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY, Chuji alisema kwamba mapema tu alijua aina ya uongozi ambao umeingia madarakani chini ya Mwenyekiti, Alhaj Yussuf Yussuf Mehboob Manji utaweka mambo sawa klabuni na timu itakuwa tishio tena.
“Unajua nilichagua jezi hii mapema kwa sababu nilijua tu msimu huu sisi hatushikiki. Wachezaji kama wanapewa kila kitu na uongozi, wanaishi katika mazingira mazuri kinachofuata ni kucheza mpira,”.
“Mimi nilitazama timu yetu ilivyo, kabisa tuna timu nzuri ambayo nilijua itafanya vizuri msimu huu. Nikasema tunachukua ubingwa, nikauliza watu wazima, utakuwa ubingwa wa ngapi, wakasema wa 24, basi hiyo ndiyo jezi yangu nitakayovaa msimu huu badala ya namba 4,”alisema Chuji ambaye tangu Polisi Dodoma anavaa jezi namba 4.
Amekuwa akivaa jezi hiyo namba nne hadi timu ya taifa, Taifa Stars na hadi msimu uliopita pia Yanga alivaa jezi hiyo.
Yanga itachuana na Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu, ambao wana Jangwani hao watakabidhiwa taji lao la ubingwa wa ligi hiyo.
Yanga japokuwa wamekwishatwaa ubingwa, lakini wamepania kushinda dhidi ya mahasimu wao hao wa jadi, ili kushangilia kwa furaha ubingwa wao.
Wazee wa Yanga juzi waliibuka kwenye vyombo vya habari na kusema ubingwa bila kumfunga Simba haunogi na kama watafungwa hawatafanya sherehe yoyote Uwanja wa Taifa Jumamosi.
Yanga pia wanakabiliwa na shinikizo la kulipa deni la kufungwa 5-0 na mahasimu wao hao wa jadi msimu uliopita katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo Uwanja huo huo.
“Bila shaka jezi ya Chuji na taji la 24 la ubingwa wa Ligi Kuu Yanga ni vitu ambavyo vinakwenda sambamba. Jezi namba 24, ubingwa wa 24. Vaa kama Chuji Jumamosi Taifa,”alisema motto huyo wa winga wa zamani wa CDA ya Dodoma, Iddi Athumani.