• HABARI MPYA

    Monday, May 13, 2013

    KUELEKEA TUZO ZA KILI 2013 KIKWETUKWETU, NANI MSANII WA KIKE, KIUME WA BENDI?

    Luiza Mbutu kulia, Jose Mara kushoto

    Na Princess Asia, IMEWEKWA MEI 13, 2013 SAA 5:31 ASUBUHI
    ZOEZI la upigaji wa kura za tuzo za wanamuziki bora Tanzania, maarufu kama Kilimanjaro Music Award lililoanza Mei 2, mwaka huu linazidi kupamba moto kwa wapenzi wa muziki kuwapigia kura wasanii wawapendao.
    Jana kwa muhtasari tulielezea ushindani uliopo katika vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa Kike Bongo Fleva, ambako kwa wanaume, Ally Kiba anachuana na Ben Pol, Diamond, Linex na Ommy Dimpoz, wakati kwa wanawake Linah anapambana na Mwasiti, Recho na Shaa.
    Awali ya hapo, tulitazana pia vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa Kike Taarabu, ambako  Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Khadija Yussuf na Leila Rashid wanawania Umalkia na akina Ahmed Mgeni, Hashim Said na Mzee Yussuf wanapigania Ufalme.
    Kabla ya hapo, tulitazama vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa Kike kwa ujumla, ambavyo vinawashindanisha Ben Pol, Diamond, Linex, Mzee Yussuf na Ommy Dimpoz kwa ‘wakaka’, wakati Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Lady Jaydee, Mwasiti na Recho watawania tuzo ya Msanii Bora wa Kike.
    Ikumbukwe tulianza na kutazama kipengele cha wimbo bora wa mwaka ambako Rapa Kala Jeremiah, kupitia wimbo wake Dear God anachuana na kundi la Kigoma All Stars na wimbo wao Leka Dutigite, Mwasiti aliyemshirikisha Ally Nipishe katika wimbo Mapito, Ommy Dimpoz aliyemshirikisha Vanessa Mdee katika wimbo Me n U na Ben Pol katika wimbo Pete.
    Leo tunahamia kwenye vipengele vya Msanii Bora wa Kiume na wa kike wa Bendi. Kwa wananaume, Chaz Baba anachuana na Dogo Rama, Greyson Semsekwa, Jose Mara na Khaleed Chokora na kwa msanii wa kike itakuwa kati ya Anneth Kushaba, Luiza Mbutu, Mary Lucos na Vumilia.
    Wasanii wote walioingia kuwania tuzo hizo ni ambao kwa hakika mwaka jana walitamba katika medani ya muziki nchini. Ni wasanii wanaobeba maana halisi ya Usanii bora- kutokana na kazi na wajihi wao.
    Hakika kuna ushindani mkubwa katika vipengele hivi na zaidi msanii atabebwa na idadi ya kura atakazopigiwa na mashabiki wake ili aweze kushinda tuzo hiyo. 
    Wapiga kura wanatakiwa kuandika namba ya msanii, wimbo, kikundi au bendi anayotaka ishinde na kisha kutuma kwenda namba 15346, wakati njia nyingine zaidi ya ujumbe mfupi (SMS) ni pamoja na Email, kwenda ktma@innovex.co.tz au kutembelea tovuti ya www.kilitimetz.com na kupiga kura moja kwa moja.
    Meneja wa Bia Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba, wamejiandaa vizuri mwaka huu kuhakikisha zoezi linafana.
    Kilele cha sherehe za utoaji tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards zilizobeba kaulimbiu ya Kikwetu kwetu ni Juni 8, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, ambako pamoja na wasanii mbalimbali kupokea tuzo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali pia. 
    Je, katika Msanii Bora wa Kike na wa Kiume  katika Bendi, utampa nani na nani kura zako?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KUELEKEA TUZO ZA KILI 2013 KIKWETUKWETU, NANI MSANII WA KIKE, KIUME WA BENDI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top