• HABARI MPYA

    Monday, May 06, 2013

    STEWART HALL: BILA AGGREY MORRIS NA NYONI UKUTA AZAM UCHOCHORO HATA KWA VIBONDE

    Kocha Stewart kulia akiwa na Msaidizi wake, Kali Ongala

    Na Mahmoud Zubeiry, Dubai
    AZAM FC imetolewa katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1 na AS FAR Rabat ya Morocco. Azam, ilianza kwa sare ya bila kufungana na timu hiyo ya jeshi la Morocco mjini Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa marudiano Rabat juzi. Je, kocha Muingereza wa Azam, Stewart Hall anasemaje baada ya matokeo hayo na ni nini mipango yake ya baadaye? Fuatilia mahojiano haya baina ya mwalimu huyo na BIN ZUBEIRY yaliyofanyika jana mjini Dubai, UAE Azam ikiwa njiani kurejea Dar es Salaam.
      
    BIN ZUBEIRY: Kocha pole kwa matokeo, najua yamekuumiza sana.
    STEWART: Dhahiri, hii ilikuwa mechi yetu kabisa, tulistahili kushinda.
    BIN ZUBEIRY: Tatizo ni nini? 
    STEWART: Bahati, bahati ndiyo kikubwa. Haikuwa bahati yetu. 
    BIN ZUBEIRY: Kwa sababu gani bahati?
    STEWART: Ooh, ulikuwa mchezo wetu. Tulipata penalti dakika ya 81, ambayo tungeshinda tungefuzu. Tukapoteza. Utasemaje? Haikuwa bahati yetu. 
    BIN ZUBEIRY: Mpigaji wa penalti yenu (John Bocco) alikuwa chaguo sahihi?
    STEWART: Ndiyo, Bocco ni mfungaji mzuri wa mipira tofauti. Na siku hiyo alitangulia kufunga kwa mpira wa adhabu. Haya mambo yanatokea katika soka, mchezaji muhimu na tegemeo, anaiangusha timu. Nani katika wachezaji wakubwa unayemjua hakuwahi kukosa penalti muhimu?
    BIN ZUBEIRY: Lakini uliruhusu mabao mawili katika mechi hiyo, hilo unalizungumziaje?
    STEWART: Sawa, upande mwingine safu yangu ya ulinzi iliniangusha. Ilifanya makosa, ambayo Rabat waliyatumia. Siwezi kumtupia lawama yeyote, ni wachezaji hawa hawa wameifikisha timu hapa. Ndiyo maana nasema haikuwa bahati yetu. 
    BIN ZUBEIRY: Unazizungumziaje kadi nyekundu walizopewa wachezaji wako?
    STEWART: Kwa Mwantika (David), sawa. Lakini ya Waziri (Salum) haikuwa sahihi.
    BIN ZUBEIRY: Kwa hiyo na refa pia alikuangusha? 
    STEWART: Ndiyo, kaniangusha. Lakini bado nasistiza siwezi kumlaumu refa aliyeipa timu yangu penalti zimebaki dakika tisa. Penalti ambayo tungefunga tungewatoa wapinzani wetu. Kwa kiasi kikubwa ninalia na bahati.  
    BIN ZUBEIRY: Umesema safu ya ulinzi ilikuangusha, ni kwenye mechi hiyo tu au imekuwa na makosa siku zote? 
    STEWART: Kwa kweli nina tatizo kwenye safu ya ulinzi kwa ujumla. Kwa sababu tunaweza kufungwa hata na African Lyon, inapitika kwa urahisi.
    BIN ZUBEIRY: Nini suluhisho la tatizo hilo?
    STEWART: Himid Mao alikuwa kiungo, ndiyo nikamrudisha beki. Mwantika ni kijana anayechipukia, yuko mafundishoni Azam. Tunamfundisha soka kwa sasa. Anatakiwa afundishwe taratibu bila kupewa majukumu mazito.
    BIN ZUBEIRY: Maana yake nini hapa?
    STEWART: Kuna wachezaji wanne (Deo Munishi, Said Mourad, Aggrey Morris na Erasto Nyoni) waliokuwa wamesimamishwa, hawa wanarudi kuboresha safu ya ulinzi na itakuwa imara tena.
    BIN ZUBEIRY: Kwa hivyo utabadalilisha safu nzima ya ulinzi?
    STEWART: Hapana.
    BIN ZUBEIRY: Bali?
    STEWART: Kuna watu ambao lazima waingie kama Aggrey na Nyoni. Lazima wacheze mechi zilizobaki za Ligi Kuu kwa sababu walicheza vizuri mechi iliyopita ya ligi (dhidi ya Coastal Union 1-1).
    BIN ZUBEIRY: Msimu umeisha, umekosa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo, unasemaje?
    STEWART: Simba na Yanga, hilo ndilo tatizo la Tanzania. Ukitazama takwimu za Ligi Kuu, utagundua Azam ilikuwa inacheza katika mazingira magumu, na Yanga walikuwa wanacheza katika mazingira mepesi. Wamefanikiwa. Lakini kama Tanzania inataka maendeleo ya kweli katika soka, lazima iepukane na haya mambo, waache soka ichezwe na bingwa apatikane kwa halali. Kwa uwezo wake.
    BIN ZUBEIRY: Msimu unaisha na mwakani utarudi katika Kombe la Shirikisho, nini kinachofuata?
    STEWART: Kumalizia mechi zilizobaki za Ligi Kuu, baada ya hapo kuitazama na kuifanyia tathmini timu. Kama tutahitaji wachezaji wa kuongeza tutajua, kama tutapunguza wachezaji, tutajua.  
    BIN ZUBEIRY: Naona kama unahitaji watu wa kuongeza katika safu ya kiungo baada ya kuondoka kwa Abdulhalim Humud?
    STEWART: Hapana, sihitaji kiungo. Kuna watu wa kutosha.
    BIN ZUBEIRY: Pale mbele kama Sure Boy (Salum Abubakar) anakosekana, inakuwaje?
    STEWART: Yupo Mieno (Humphrey) 
    BIN ZUBEIRY: Huyo unamtumia kama mshambuliaji pamoja na John Bocco kwa sasa…
    STEWART: Namtumia huko kwa muda tu, wakati natafuta namna bora ya kumtumia, ila yule ni kiungo na mchezaji mzuri sana. Amefunga mabao manne.
    BIN ZUBEIRY: Unasemaje kuhusu Brian Umony? 
    STEWART: Ni mchezaji mzuri, maumivu yalipunguza kasi yake, lakini nina matarajio makubwa na yeye msimu ujao.
    BIN ZUBEIRY: Dida (Deo Munishi) anarudi kikosini, wakati huo huo Mwadini Ally na Aishi Manula wote ni makipa wa timu ya taifa, itakuwaje?
    STEWART: Hiyo ni changamoto kwao wote, unasahau kumtaja Wandwi (Jackson), naye ni kipa mzuri, watakuwa wanne na nitampa nafasi mtu kutokana na uwezo wake, si kitu kingine.
    BIN ZUBEIRY: Chini yako, Azam inahitaji muda gani zaidi kutwaa ubingwa wa Bara?
    STEWART: Tunajifunza kila msimu, nadhani somo la msimu huu linatosha, nina matarajio makubwa ya kufanya hivyo msimu ujao. 
    BIN ZUBEIRY: Kipi kinakupa imani hiyo?
    STEWART: Uwezo wa timu unavyozidi kukua kila siku.
    BIN ZUBEIRY: Simba na Yanga nazo zinazidi kujiimarisha. 
    STEWART: Najua, na sidharau. Ila nazungumzia timu yangu. 
    BIN ZUBEIRY: Kwa leo niseme inatosha na ninashukuru kocha. Kazi njema.
    STEWART: Asante. Karibu tena.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: STEWART HALL: BILA AGGREY MORRIS NA NYONI UKUTA AZAM UCHOCHORO HATA KWA VIBONDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top