• HABARI MPYA

    Friday, June 07, 2013

    MISS KIGAMBONI NI LEO NAVY BEACH, BRIGITTE KUVULIWA TAJI MISS SINZA

    Brigitte Alfred
    Na Princess Asia, IMEWEKWA JUNI 7, 2013 SAA 1:00 ASUBUHI
    WAKATI Redd’s Miss Kigamboni akitarajiwa kupatikana leo usiku, pia wengi watataka kujua nani atafanikiwa kumvua taji la kwanza Redd’ Miss Tanzania, Brigette Alfred katika kinyang’anyiro cha kuwania taji la Redd’s Miss Sinza.
    Redd’s Miss Tanzania, Brigette ndiye Redd’s Miss Sinza, hivyo leo ataanza rasmi kuvua mataji anayoshikilia pale atakapomkabidhi taji hilo mrembo atakayepatikana baadaye usiku.
    Shindano la Redd’s Miss Sinza linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Meeda uliopo Sinza, huku lile la Redd’s Miss Kigamboni ambalo nalo litakuwa na mambo kibao linatarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni, Dar es Salaam.
    Akizungumzia shindano la Redd’s Miss Sinza, Mratibu wa kinyang’anyiro hicho, Majuto Omary alisema kila kitu kimekamilika, huku bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ wakitarajiwa kutoa burudani.
    Naye Redd’s Miss Tanzania, Brigitte Alfred alisema haoni sababu ya warembo wa kitongoji hicho kushindwa kufanya vizuri kwani amewaona na anaamini wana uwezo mkubwa.
    “Sioni sababu ya kushindwa kufanya vyema katika mashindano haya, Redds Miss Sinza ndiyo inatetea taji la Miss Kinondoni na Miss Tanzania pia, hivyo macho ya wadau wote wa urembo yatakuwa kwenu, mnatakiwa kujituma na kuwafanya majaji kuwa na kazi ya ziada kumpata mshindi,” alisema Brigitte.
    Naye Mratibu wa shindano la Redd’s Miss Kigamboni, Somoe Ng’itu alisema warembo wao wamejiandaa vyema na kutakuwa na burudani ya kufa mtu kutoka kwa FM Academia iliyo chini ya Nyoshi El Saadat.
    “Kuna warembo 12 ambao watapanda jukwaani na watu wajitokeze kwa wingi ili kumshuhudia Redd’s Miss Kigamboni, ambaye tuna uhakika atakuwa Redd’s Miss Tanzania,” alisema Somoe.
    Wakati Redd’s Miss Sinza na Kigamboni kukiwa na shughuli pevu, pia kazi kubwa ipo kwa Redd’s Miss Mara, ambapo napo kutakuwa na kinyang’anyiro cha kumpata mrembo wa mkoa huo leo.
    Shindano hilo linatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Musoma Club, huku kukiwa na burudani za kufa mtu itakayotolewa na kundi la Homeland Stars.
    Kinyang’anyiro hicho kinatarajiwa pia kuendelea kesho katika maeneo kadhaa ambapo kutakuwa na kazi ya kumsaka Redd’s Miss mbeya, Redd’s Miss Arusha, Redd’s Miss Kigoma na Redd’s Miss Shinyanga.
    Shindano la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MISS KIGAMBONI NI LEO NAVY BEACH, BRIGITTE KUVULIWA TAJI MISS SINZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top