IMEWEKWA JUNI 7, 2013 SAA 7:30 USIKU
MTENDAJI Mkuu wa Arsenal, Ivan Gazidis amethibitisha kwamba anataka Arsene Wenger aongeze Mkataba wake mwishoni mwa msimu ujao na kuiongoza klabu hiyo kufanya vizuri katika soka ya Ulaya.
Mkataba wa Wenger unaisha mwakani na tayari amepelekewa ofa kibao kuanzia nyumbani kwao Ufaransa, ambako Paris Saint-Germain na klabu yake ya zamani, Monaco zinamtaka.
Gazidis (chini kushoto) anataka Mfaransa aongeze Mkataba mwishoni mwa msimu ujao
Matokeo mabaya ya miaka ya karibuni yalitarajiwa kumuweka katika wakati mgumu kocha huyo mwenye umri wa miaka 63, lakini Gazidis anatarajia atabaki na kuunda kikosi cha nguvu.
Pato la mwaka la Arsenal linatarajiwa kuongezeka kwa Pauni Milioni 70, na kuwasogeza kwa wanaopata Pauni Milioni 300, Real Madrid, Barcelona, Manchester United na mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich.
Hiyo itawapa fursa ya kushindana na klabu hizo kununua wachezaji wa kuanzia Pauni Milioni 25 na kutaka mishahara ya kuanzia Pauni 200,000 kwa wiki kama Wayne Rooney, mmoja kati ya wachezaji inayowataka hivi sasa.
Klabu tatu za juu katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, Manchester United, City na Chelsea zote zimebadilisha makocha wao, lakini Arsenal bado na imani na Wenger.