IMEWEKWA JULAI 15, 2013 SAA 2:30 ASUBUHI
KLABU ya Arsenal imeendeleza dhamira ya kumsajili Luis Suarez na wiki hii itapanda dau hadi Pauni Milioni 35 kwa ajili ya nyota huyo wa Liverpool anayetaka kuondoka.
Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Uruguay kwa sasa ni chaguo namba moja la Arsene Wenger katika usajili wa majira haya ya joto na iko tayari kutoa dau kumhamishia Emirates Stadium.
Arsenal imeshuhudia ofa yao ya awali ikipigwa chini Merseysiders, ambayo inataka Pauni Milioni 40 angalau ili kumuuza nyota huyo wa Amerika Kusini.
Anatakiwa: Arsenal imetuma maombi ya Liverpool kwa ajili ya kumsajili Suarez, wakati mustakabali wa nyota huyo wa Uruguay ni tata
Wakiwa wameona dau lao la Pauni Milioni 30 limepigwa chini, The Gunners itampandia dau mchezaji huyo wiki hii.
Matumaini yanakuwa kwa wapenzi wa Arsenal kwamba, dili hilo si masihara na klabu itatumia sehemu ya Pauni Milioni 70 ilizotenga kwa ajili ya usajili kumnasa Suarez.
Wenger anakabiliwa na changamoto ya kusajili mshambuliaji wa kiwango cha dunia majira haya ya joto baada ya taarifa tofauti kusema kwamba klabu ipo katika nafasi nzuri kifedha kusaini kipoaji cha hali ya juu.
Dau la Pauni Milioni 23 kwa ajili ya kumsaini Gonzalo Higuain, ambaye atarejea kwenye mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya Real Madrid leo, kimsingi limekubaliwa.
Mguu nje: Liverpool inataka Pauni Milioni 40 kwa ajili ya mshambuliaji huyo wa Uruguay, lakini Arsenal haina dalili za kufika bei hiyo
Na vyovyote itakavyokuwa juu ya dili la kumsaini Muargentina huyo, Wenger ameelekeza nguvu zake zaidi katika kuwania saini ya Suarez, ambaye atakosa mechi sita za mwanzo wa msimu.
Lakini Arsenal si klabu pekee inayomtaka Suarez, kwani hata Real Madrid na Manchester City zinamhitaji pia. Suarez mwenyewe amekwishaweka wazi anataka kuondoka Liverpool aende klabu ambayo atakuwa anacheza Ligi ya Mabingwa.
Arsenal ilianza vyema ziara ya kujiandaa na msimu mpya baada ya kuichapa 7-0 Dream Team ya Ondinesia mjini Jakarta jana. Olivier Giroud alifunga mabao mawili, mengine Chuba Akpom, Theo Walcott, Lukas Podolski, Kris Olsson na Thoms Eisfeld.