• HABARI MPYA

    Thursday, July 18, 2013

    SIMBA SC YAMTAKA MWINYI KAZIMOTO AJISALIMISHE VINGINEVYO...

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 18, 2013 SAA 6:16 MCHANA
    SIMBA SC imemtaka kiungo wake Mwinyi Kazimoto Mwitula kuibuka kutoka mafichoni alipo ili imsaidie kufanikisha mipango yake ya kwenda kucheza Qatar, alipopata nafasi, vinginevyo watamshitaki Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Kazimoto alitoroka kwenye kambi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars baada ya mchezo wa kwanza na Uganda kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee Jumamosi iliyopita mjini Dar es Salaam.
    Wakati Stars inakwenda kuweka kambi mjini Mwanza kujiandaa na mchezo wa marudiano wikiendi ijayo, ndipo ikagundulika Kazimoto ametoweka na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likasema halitampatia kibali cha kucheza huko kwa kitendo hicho cha kutoroka.
    Jisalimishe; Kiungo Mwinyi Kazimoto ametoweoka kwenda Qatar na klabu yake imemtaka ajisalimishe

    Lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amemtumia salamu kiungo huyo wa zamani wa JKT Ruvu, akimuambia; “Hana haja ya kutoroka, aje tumsaidie kufanikisha safari yake,”.
    Poppe amesema sera ya Simba SC inafahamika wazi ni kutowabania wachezaji wanaopata nafasi za kwenda kucheza nje, hivyo wanastaajabu kitendo cha Mwinyi kutoroka baada ya kuomba ridhaa na msaada wa klabu yake.
    “Popote alipo Mwinyi na hata hao watu wanaotaka kumpeleka Qatar, tunawaomba wasilifanye hili suala likawa gumu, waje tuzungumze na tuwasaidie kumpata huyo mchezaji kwa njia za halali,”alisema.
    Ajitokeze haraka; Hans Poppe amemtaka
    Kazimoto ajitokeze wayamalize aende Qatar

    Alipoulizwa kwamba labda atahofia mkwara wa TFF, Poppe alisema; “TFF inaongozwa na watu watu wazima na weledi, ambao wanaelewa matatizo na shida za wachezaji wetu, kama Mwinyi na hao wanaotaka kumpeleka Qatar watakuja kwetu, tutayamaliza yote Na atakwenda kucheza popote na ataendelea kuwa mchezaji wa timu ya taifa, “alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).  
    Poppe amesema iwapo ndani ya siku tatu hawatasikia wala kuona lolote juu ya mchezaji huyo, wataanza rasmi taratibu za kuripoti Shiriksho la Soka la Kimataifa (FIFA) na kuwataja watu wanaotuhumiwa kuhusika katika mpango huo, ili wachukuliwe hatua.
    “Huyu mchezaji ana mkataba na sisi, kuondoka kwenda sehemu yoyote bila ruhusa ya klabu yake ni kosa kisheria. Na hao mawakala au watu wanaotaka kumchukua kinyume cha sharia, FIFA haitawanusuru, wakae wakijua hilo,”alionya Poppe.
    Ameongeza; “Sisi hatuna tatizo, wachezaji wetu wangapi tumewaruhusu kucheza nje, wengi tu. Mbwana Samatta, Patrick Ochan (TP Mazembe, DRC), Danny Mrwanda (Vietnam), Emmanuel Okwi (Etoile du Sahel, Tunisia) na Shomary Kapombe sasa anaenda Uholanzi, sasa huwezi kuona mantiki ya Mwinyi kutoroka,”alisema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC YAMTAKA MWINYI KAZIMOTO AJISALIMISHE VINGINEVYO... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top