• HABARI MPYA

    Sunday, July 07, 2013

    YANGA SC YAPIGWA 2-1 NA EXPRESS SHINYANGA...MBUYU TWITE, KAVUMBANGU, TEGETE, BAHANUZI WOTE NDANI...DIDA AWEKA REKODI YA KUFUNGWA MABAO MATATU MECHI MBILI

    Na Prince Akbar, IMEWEKWA JULAI 7, 2013 SAA 1:17 USIKU
    YANGA SC imefungwa mabao 2-1 na Express ‘Red Eagles’ ya Uganda katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na msimu mpya Uwanja wa Kambarage Shinyanga.
    Huo ulikuwa mchezo wa marudiano baada ya jana timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.  
    Tai Wekundu wa Kampala leo ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Mussa Mukasa dakika ya 10, kabla ya Shaaban Kondo aliyesajiliwa kutoka Msumbiji kuisawazishia Yanga dakika ya 30. 
    Yanga SC

    Bao hilo lilitokana na mpira wa kurushwa wa beki Mbuyu Twite ambao uliongezewa kasi na Abdulrahman Sembwana aliyepandishwa kutoka timu B kabla ya Shaaban 
    Kondo kumalizia kwa kuusukumia nyavuni.
    Hata hivyo, mfungaji wa bao la Express jana Kavuma Winny aliiua Yanga leo dakika ya 77 kwa bao safi la pili, akifanya kipa mpya wa wana Jangwani hao, Deo Munishi ‘Dida’ aliyesajiliwa kutoka Azam FC, awe amefungwa mabao matatu katika mechi mbili.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Mbuyu Twite, Bakari Masoud/Salum Telela, Andulrahman Sembwana/Abdallah Mnguli, Hamisi Thabit/Nizar Khalfan, Shaaban Kondo/Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi/Notikel Masasi na Sospeter Mhina/Jerry Tegete.
    Yanga inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts inatarajiwa kucheza mechi ya mwisho katika ziara yake ya Kanda ya Ziwa Julai 11 mjini Tabora kabla ya kurejea Dar es Salaam kuendelea na maandalizi yake ya msimu mpya.
    Awali, Yanga ilitarajiwa kumenyana na mabingwa wa Uganda, KCC lakini kutokana na sababu ambazo hazikuelezwa, Wafagia Barabara wa Kampala hawakuja na imecheza na mabingwa wa zamani wa nchi hiyo, Tai Wekundu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC YAPIGWA 2-1 NA EXPRESS SHINYANGA...MBUYU TWITE, KAVUMBANGU, TEGETE, BAHANUZI WOTE NDANI...DIDA AWEKA REKODI YA KUFUNGWA MABAO MATATU MECHI MBILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top