• HABARI MPYA

    Sunday, August 18, 2013

    JOHN BOCCO 'ADEBAYOR' AONDOKA AKICHECHEMEA TAIFA, KUWAKOSA MTIBWA SUGAR MANUNGU

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA AGOSTI 18, 2013 SAA 1:00 ASUBUHI
    HALI imezidi kuwa mbaya Azam FC baada ya idadi ya majeruhi sasa kufika watatu, kufuatia John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kuumia katika mchezo wa jana kuwania Ngao ya Jamii, timu yake ikilala 1-0 mbele ya Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Bocco aliondoka uwanjani akichechemea jana, huku akisaidiwa na mchezaji mwenzake, Himid Mao baada ya kuumia na kutoka uwanjani dakika ya 74 akimpisha Gaudence Mwaikimba.
    Bocco aligongana na beki wa Yanga SC, Mbuyu Twite dakika ya 71 na akajaribu kuinuka, akakaa tena chini kabla ya kubebwa na kutolewa nje kwa huduma ya kwanza.
    Aligongwa sana tu jana; John Bocco jana aligongwa sana na wachezaji wa Yanga kama inavyoonekana hapa akikanyagwa na Nadir Haroub 'Cannavaro'

    Alirejea uwanjani dakika moja baadaye baada ya kutibiwa, lakini akaonekana kabisa hayuko vizuri na kocha Muingereza, Stewart John Hall akamuingiza Mwaikimba kuchukua nafasi yake.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY wakati anaelekea kwenye gari la timu yake, Bocco alisema kwamba hatarajii kama yatakuwa maumivu makubwa, lakini yanaweza kumuweka nje ya Uwanja angalau kwa wiki moja.
    “Siyo sana, ila naweza kuwa nje kwa wiki moja hivi. Maana nasikia maumivu na ndiyo maana nimeshindwa kumalizia mechi,”alisema.
    Alimtoa nje Yondan; John Bocco 'Adebayor' aligongana na Yondan hadi akatoka nje



    Mashabiki wa Yanga SC walifurahia kuumia kwa Bocco hadi kutoka nje, kwa sababu kabla ya hapo naye aligongana na beki wao, Kevin Yondan hadi akatoka nje dakika ya 11.
    Wengi waliamini pia Bocco ndiye aliyegongana na kipa wa Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ hadi akatoka nje dakika ya 15, ingawa tukio hilo lilimuhusisha Kipre Tchetrche. 
    Bocco sasa anaungana na majeruhi wengine wa timu hiyo, Brian Umony na Humphrey Mieno na anaweza kuukosa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro mwishoni mwa wiki ijayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: JOHN BOCCO 'ADEBAYOR' AONDOKA AKICHECHEMEA TAIFA, KUWAKOSA MTIBWA SUGAR MANUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top