• HABARI MPYA

    Wednesday, November 20, 2013

    MBOMOA SIMBA NI MWANASIMBA, NA NDIYE…

    MIGOGORO ni sumu ya maendeleo katika jambo lolote, si michezo pekee na wakati mwingine husababisha upotevu wa amani.
    Soka ya Tanzania kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na migogoro, kwa sababu watu wanatumia muda mwingi kupambana na kulumbana badala ya kufanya shughuli za maendeleo.
    Moja kati ya mambo ambayo yatafanya Leodegar Chilla Tenga akumbukwe daima pamoja na kuwa mchezaji hodari wa nafasi ya ulinzi enzi zake, pia ni kutengeneza mfumo bora wa uongozi katika soka yetu unaosaidia kuepukana na migogoro.

    Sasa soka yetu inaongozwa kwa misingi mizuri ya Katiba, taratibu na sheria, hivyo zile zama za viongozi kupinduliwa na vurugu zisizo na kichwa wala miguu tumekwishaondokana nazo.
    Lakini siku zote, klabu mbili kubwa nchini Simba na Yanga ndizo zimekuwa chanzo cha matatizo yetu- kwa sababu kwao imekuwa vigumu kuheshimu taratibu hizo.
    Na kwa sababu hiyo soka ya Tanzania haiendi popote haswa ikizingatiwa klabu hizo mbili ndizo mihimili mikubwa ya soka yetu. Zenyewe zipo zipo tu ili mradi zisukume siku na hazina jipya wala hazina matarajio yoyote.
    Hivi sasa katika klabu ya Simba kuna mgogoro unafukuta, baina ya Mwenyekiti, Alhaj Ismail Aden Rage na viongozi wenzake wa Kamati ya Utendaji.
    Rage anatuhumiwa kufanya mambo mengi bila kushirikisha wenzake na katika maamuzi yake mengi, ni ambayo yanaiingiza klabu katika matatizo.
    Kwa sababu hiyo, kikao cha Kamati ya Utendaji kilichokutana juzi bila ya Rage kuwepo, kikaamua kumsimamisha hadi hapo Mkutano Mkuu wa wanachama utakapoitishwa kukutana kumjadili.
    Rage ni mpiganaji, hilo linafahamika na baada ya kimya ataibuka kupambana na wenzake na atajipanga hata kwenye Mkutano Mkuu kama itabidi kujadiliwa, akashinde.
    Kwa kuwa hapa kuna pande mbili zinazopingana, tayari huu ni mgogoro na tunajua fika, Rage ni mbishi, mjuaji na mpambanaji- hivyo kama wenzake nao wataamua kupambana naye kweli, hii itakuwa vita nzito na mwisho wa siku itakayoathirika ni klabu.
    Rage amekuwa akipingwa kwa muda mrefu Simba SC na wakati wote amekuwa akipambana na kwa hali hiyo huwezi kustaajabu hakuna cha maana alichokifanya hadi sasa yeye na Kamati yake ya Utendaji tangu waingie madarakani.
    Wapo wanachama wa klabu hiyo wanaofurahia hali ya migogoro katika klabu hiyo, kwa sababu ni fursa nzuri kwao kujipatia riziki kwa njia za upambe na kuzidi kuchochea moto klabuni.
    Ni hali ambayo inasikitisha na hii ni desturi sugu ndani ya klabu hizi- hakuna kiongozi alikaa madarakani hakupingwa, hakupewa kashfa za wizi na kadhalika- kila kiongozi huwa anafaa anapochaguliwa tu, lakini anapoingia ofisini hafai- na sidhani kama hii itaisha.
    Hassan Daalal alipata misukosuko mingi alipokuwa madarakani, naye alipambana hadi ulipowadia wakati akamuachia Rage. Zamani tulikuwa tuna usemi; Mjenga nchi ni mwananchi, na mbomoa nchi ni mwananchi, vyema wana Simba nao wakafahamu, mjenga Simba ni mwanasimba, na mbomoa Simba ni mwanasimba, sasa wamue kuijenga au kuibomoa klabu yao. Jumatano ya heri kwa wote. Asanteni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBOMOA SIMBA NI MWANASIMBA, NA NDIYE… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top