• HABARI MPYA

    Sunday, August 17, 2014

    FIFA YAMRUDISHA MALINZI KARUME, TFF YATEMA OFISI ZA BEI MBAYA DAR ES SALAAM MJINI

    Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Miguu Tanzania (TFF) limeamua kurejesha ofisi zake Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kwa vile mipango ya uendelezaji wa eneo hilo bado haijakwenda kama ilivyopangwa awali.
    Uamuzi huo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa kati ya Kamati ya Utendaji ya TFF na ujumbe wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) uliokuwepo nchini kwa wiki nzima kwa ajili ya kufanya mapitio (review) ya uendeshaji wa TFF.
    Akizungumza Dar es Salaam leo (Agosti 17 mwaka huu), kiongozi wa ujumbe huo wa FIFA uliokuwa na maofisa sita, Zelkifli Ngoufonja amesema wamepitia maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa TFF na mpira wa miguu kwa ujumla na kukubaliana kufanya uboreshaji kwa lengo la kuongeza ufanisi.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi kulia akiwa na Rais wa FIFA, Sepp Blatter kushoto

    Ngoufonja ambaye ni Meneja Mwandamizi wa FIFA anayeshughulikia Programu za Maendeleo Afrika amesema kabla walikutana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kwa lengo la kuangalia jinsi watakavyochangia katika uendelezaji mpira wa miguu nchini.
    Amesema wamekubaliana na TFF katika mpango wa utekelezaji (Action Plan) na maazimio waliyokubaliana ikiwemo na muda wa utekelezaji wake, hivyo FIFA watafuatilia na kutoa msaada ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kama ilivyopangwa.
    Maeneo yaliyofanyiwa kazi ni utawala bora (Governance), Maendeleo ya Ufundi (Technical Development), timu za Taifa (National teams), Mashindano na Vitendea Kazi (Competitions and Facilities), na Utawala na Uongozi (Administration and Management).
    Maofisa wengine wa FIFA waliofuatana na Ngoufonja ambaye ni raia wa Cameroon ni Meneja wa Programu za Ustawi (Performance), Marco Schuepp, Ofisa Maendeleo, Ashford Mamelodi, Ofisa Maendeleo wa Ufundi, Govinden Thondoo, Mkufunzi wa Makocha, John Peacock na Mshauri wa Programu za Ustawi, Ian Riley.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FIFA YAMRUDISHA MALINZI KARUME, TFF YATEMA OFISI ZA BEI MBAYA DAR ES SALAAM MJINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top