• HABARI MPYA

    Wednesday, June 03, 2015

    KICHEFUCHEFU KITUPU KUANZIA FIFA, CAF, TFF, KLABU NA WACHEZAJI WENYEWE!

    KATIKA siku ambayo Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Sepp Blatter alikuwa anatangaza nia ya kuachia ngazi- nchini Tanzania klabu ya Simba SC ilikuwa inatangaza dhamira ya kumchukulia hatua mchezaji wake Ramadhani Singano ‘Messi’. 
    Jana, ikiwa ni siku tano tangu Blatter achaguliwe tena kwa mara ya tano kuendelea kuongoza FIFA, amesema atang’atuka na Simba SC ikasema itamchukulia hatua Messi kwa kuwatuhumu kughushi Mkataba wake.
    Katika taarifa iliyotolewa jana makao makuu ya FIFA mjini Zurich, Uswisi, Blatter amesema anaondoka baada ya miaka 17 kama mtu wa nguvu katika soka. Blatter amesema; "Nitaendelea na nafasi yangu FIFA hadi wakati ujao. Uchaguzi mpya utafanyika Mexico,". 
    Blatter kwa sasa yuko chini ya uchunguzi mkali wa FBI kama bodi hiyo ya soka ilihusika na rushwa. 
    Idara ya Sheria ya Marekani imesema dola za Kimarekani Milioni 10 walipewa Wajumbe wa zamani wa FIFA, Jack Warner na Chuck Blazer kutoka akaunti ya FIFA katika benki ya Uswisi mwaka 2008.
    Gazeti la New York Times limesema kwamba malipo hayo yalifanywa na Katibu Mkuu, Jerome Valcke. Valcke amekana madai hayo na Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Habari ya FIFA, Delia Fischer amesema ni Julio Grondona aliyefanya malipo hayo.
    Baadaye ikagundulika Valcke alikuwa anafahamu kuhusu malipo hayo. FIFA imeitisha Mkutano baadaye na Blatter anajiandaa kuhudhuria. 
    Malipo hayo ambayo yanafanyiwa uchunguzi na FBI, inadaiwa fedha hizo walilipwa Makamu wa Rais wa zamani wa FIFA, Jack Warner na Msaidizi wake Chuck Blazer kama malipo yao kwa kuichagua Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.
    Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki amekanusha nchi yake kuhonga ili kupata uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia.  
    Blatter amekiri tuhuma hizo hizo zimechafua kila kitu katika miaka yake 17 ya kuongoza soka kwa ufanisi wa hali ya juu na babu huyo wa umri wa miaka 79, ambaye alishinda tena uchaguzi wa FIFA Ijumaa kwa mara ya tano licha ya tuhuma hizo, amekanusha kuwa muhusika wa sakata hilo ambaye hakutajwa jina.
    "Hakika siyo mimi," Blatter alisema katika Mkutano na Waandishi wa Habari Jumamosi. Warner, ni miongoni mwa Maofisa 14 wa FIFA waliofunguliwa mashitaka na Idara ya Sheria ya Marekani Jumatano iliyopita kwa tuhuma za rushwa ya zaidi ya dola za Kimarekani Milioni 150.  
    Warner alitoka jela mjini Trinidad and Tobago Alhamisi na mara moja akamgeukia Blatter akihoji kwa nini naye hachunguzwi.  
    Ya FIFA ni mazito, Blatter ameiongoza vizuri tangu arithi mikoba ya Joao Havelange mwaka 1998- lakini mabadiliko aliyoyafanya katika kipindi chake cha miaka 17, ikiwemo kuutenga mchezo wa soka na mamlaka zote za dola yalikuwa yanatia shaka.
    Mazingira ya rushwa na ufisadi katika mchezo yalikuwa nje nje- na pamoja na kujiwekea ngome nzito, hatimye mtu mzima maji yamemfika shingoni na jana kasema ataachia ngazi.
    Kana kwamba haitoshi- Blatter amekiri FIFA inahitaji kuundwa upya. Imechafuka. Maana yake mchezo kwa ujumla umepoteza heshima. Uchafu unaogundulika sasa FIFA, dhahiri umeota mizizi hadi kwenye bodi za mabara kuanzia Ulaya (UEFA) hadi Afrika (CAF).
    Imeenea hadi kwenye vyama (FA) za nchi na ikasambaa hadi kwenye taasisi na kamati ndogo ndogo, zikiwemo za marefa.
    Kamari imekuja kuichafua zaidi soka- na kashfa za upangaji matokeo zimekuwa lukuki. Ndiyo, soka sasa imechafuka na inahitaji kusafishwa.
    Blatter alitumia umasikini wa nchi za Afrika kujifanya mwema kwa misaada aliyokuwa anatoa- yana mwisho, wakubwa wamembana na hatimaye amekubali kuachia chombo.
    Kukubali tu haitoshi, lakini naye amekiri soka imechafuka. Nini kitafuatia Blatter atakapokabidhi ofisi (sijui lini) na nani atakuwa mbadala wake na atakuwa msafi? Hayo ni mambo ya kusubiri na kuona.
    Wakati dunia ya soka imekumbwa na mtikisiko, nchini Tanzania nako kuna yake. Wapenzi wa soka wanalia na matokeo mabaya ya timu yao ya taifa hivi karibuni kwenye michuano ya COSAFA.
    Wanasubiri kuona hatima yao kwenye mechi za kufuzu AFCON na CHAN. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemuambia kocha Mholanzi, Mart Nooij ataondoka iwapo timu haitafuzu CHAN.
    Klabu za Tanzania zimeendelea kuzisikia tu ‘kwenye bomba’ hatua ya makundi za michuano ya Afrika na mwaka huu, kidogo Yanga SC wamejitahidi kufika hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho. Azam FC walitolewa hatua ya awali tu Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Mpya zaidi ni hii; jana Simba SC imesema inajipanga kumchukulia hatua mchezaji wake, Ramadhani Singano ‘Messi’ kwa kuituhumu klabu hiyo kughushi Mkataba wake.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ‘Zungu’ alifanya Mkutano wa kwanza na Waandishi wa Habari jana makao makuu ya klabu, Msimbazi tangu arejee kutoka Afrika Kusini kusaka vipaji kwenye Kombe la COSAFA.
    Na Manara akasema kwamba Simba haijachezea mkataba wa Messi kama anavyodai, ila wanaamini hiyo ni janja yake kwa kushirikiana na klabu inayomtaka, kutaka kumchukua bila malipo.
    “Simba inatambua mkataba wa Messi unamalizika mwakani na si mwaka huu kama anavyodai. Kama kuna klabu inamuhitaji mchezaji huyo, bora ijitokeze na kufanya mazungumzo ramsi na Simba ambayo ilimuibua nyota huyo,”amesema Manara.
    Mtoto huyo wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Sunday Manara ‘Kompyuta’, amesema kwamba pia wanashangazwa na kuibuka kwa Meneja wa Messi.
    “Huyo anayejiita Meneja wa Messi, anatambulika wapi kisheria?”alihoji na kuongeza; “Kitendo alichokifanya Messi kinafanyiwa kazi na mamlaka za ndani za Simba na baadaye tutatoa tamko la hatua tuliyochukua,”.
    Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka minne iliyopita, hivi karibuni ameibua shutuma dhidi ya klabu yake hiyo kwamba imeghushi Mkataba wake.
    Messi anadai Mkataba wake halali ulikuwa unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika mwakani.
    Na Messi si mchezaji wa kwanza kuishutumu Simba SC kughushi Mkataba wake, kwani wachezaji wengine wa zamani wa klabu hiyo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Kevin Yondan wamewahi kutoa malalamiko kama hayo wakati wanahamia kwa mahasimu, Yanga SC.
    Tumesema huko nyuma yamewahi kutokea malalamiko kama hayo dhidi ya Simba SC, wachezaji Chuji na Yondan wakidai klabu hiyo ilighushi Mikataba hiyo, lakini sakata hizo ziliishaje?
    Sote tunafahamu kughushi Mkataba ni kosa la jinai, lakini kulingana na namna ambavyo masuala ya Chuji na Yondan yalimalizwa, si ajabu yanaibuka na haya ya Messi pia.
    Kama wachezaji walikuwa waongo, walichukuliwa hatua gani. Na kama Simba SC walighushi kweli mikataba walichukuliwa hatua gani. Kama hakuna hatua zilizochukuliwa ajabu gani sasa yanaibuka tena na haya Messi? 
    Na iwapo na hili la Messi litamalizwa ‘kisamjo’ kwa nini tusijitayarishe kusikia kesi za aina hiyo siku si nyingi tena? Na hapo ndipo soka inapozidi kuchafuka. Inanuka kuanzia FIFA, CAF, CECAFA, TFF hadi klabu na wachezaji wenyewe kichefuchefu kitupu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KICHEFUCHEFU KITUPU KUANZIA FIFA, CAF, TFF, KLABU NA WACHEZAJI WENYEWE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top